Michezo

Baada ya ushindi Kasarani, jeraha kumweka nje Wanyama Spurs

October 15th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

VICTOR Wanyama ameingia katika orodha ya majeruhi ya Tottenham Hotspur baada ya kupata jeraha la misuli ya paja dhidi ya Ethiopia jijini Nairobi mnamo Oktoba 14, 2018.

Hata hivyo, madaktari wa Spurs hawajatangaza habari kuhusu ubaya wa jeraha lake, muda atakaokuwa nje ama kurejea ulingoni.

Kiungo huyu mkabaji mwenye umri wa miaka 27 alijeruhiwa katika mguu wake wa kushoto kwenye mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 ambayo nchi yake ya Kenya ilishinda Ethiopia kwa mabao 3-0 uwanjani Kasarani.

Wanyama alifunga penalti katika mechi hiyo ya Kundi ‘F’ ambayo matokeo yake yaliimarisha alama za Kenya hadi saba, pointi tatu mbele ya Ethiopia na nne mbele ya Ghana na Sierra Leone.

Mkenya huyu aliondolewa uwanjani dakika ya 73 na nafasi yake kujazwa na Johana Omolo anayesakata katika klabu ya Cercle Brugge nchini Ubelgiji.

Wanyama anaungana mkekani na Danny Rose (jeraha la kinena), Jan Vertonghen, Mousa Dembele, Dele Alli (jeraha la misuli ya paja), Christian Eriksen (jeraha la tumbo) na Vincent Janssen (jeraha la mguu).

Wanyama amecheza jumla ya dakika 53 pekee msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Uingereza. Aliumia goti Julai 24 wakati Spurs ikijiandaa kwa msimu mpya. Alikosa mechi tatu za kwanza ligini dhidi ya Newcastle United, Fulham na Manchester United kutokana na jeraha hilo. Kisha alikuwa kwenye benchi dhidi ya Watford kabla ya kupewa dakika saba dhidi ya Liverpool mnamo Septemba 15.

Alitiwa kwenye benchi tena dhidi ya Brighton kabla ya kutumiwa kwa dakika 45 dhidi ya Huddersfield hapo Septemba 29. Alishiriki dakika tano pekee katika mechi dhidi ya Cardiff mnamo Oktoba 6, ambayo ilikuwa yake ya mwisho kabla ya kuja kuwakilisha Kenya katika mechi za kufuzu kushiriki AFCON mwaka 2019.

Alikuwa katika kikosi cha Harambee Stars kilichokabwa 0-0 dhidi ya Ethiopia mjini Bahir Dar mnamo Oktoba 10. Jeraha alilopata Oktoba 14 katika mechi ya marudiano dhidi ya majirani hawa wake huenda likamfanya akose mechi ya Spurs ijayo dhidi ya West Ham mnamo Oktoba 20.