Siasa

Baadhi ya maseneta wapinga kung'atuliwa kwa Sonko

December 9th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BAADHI ya maseneta sasa wanadai kuwa ujanja wa Gavana wa Nairobi Mike Sonko wa kutoteua Naibu wake huenda ukamwokoa dhidi ya kung’olewa afisini.

Wanasema kuondolewa kwake kutasababisha kufanyika kwa uchaguzi mdogo wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa kura ya maamuzi kuhusu marekebisho ya Katiba.

Hata hivyo, wanakubalia kuwa mashtaka dhidi ya Bw Sonko ni mazito na yanaweza kuchangia kuondolewa kwake afisini.

“Hatutaki kufanyike uchaguzi mdogo wa ugavana katika kaunti ya Nairobi wakati huu. Tunataka kuepuesha suala kama hilo ambalo litapandisha joto la siasa sio tu jijini Nairobi bali kote nchini kwa sababu hili ni jiji kuu la Kenya,” akasema seneta mmoja ambaye aliomba jina lake libanwe.

Kauli kama hiyo iliungwa mkono na maseneta wanaegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto, Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Aaron Cheruiyot (Kericho) waliokuwa wakiongea Jumanne katika kaunti ya Kericho.

“Huu sio wakati wa kuondoa Gavana wa jiji kuu la Kenya afisini. Raslimali na juhudi zote zinafaa kuelekezwa mipango ya kukabiliana na changamoto zinazoisibu nchini kama vile janga la corona na kudorora kwa uchumi. Hakuna haya ya kuwasumbua wakazi wa Nairobi na uchaguzi mdogo wa ugavana,” akasema Bw Murkomen wakati wa ibada ya wafu ya marehemu Meja Jenerali John Koech katika eneobunge la Ainamoi, Kaunti ya Kericho.

Sonko amedinda kuteua Naibu Gavana tangu Bw Poliycarp Igathe alipojiuzulu mnamo Januari 2018.

Jaribio lake la kumteua Bi Anne Kananu Mwendwa mwaka 2019 lilikabiliwa na changamoto baada ya mchakato wa kumpiga sasa kusimamishwa na Mahakama Kuu

Kulingana na sehemu ya 32A ya Sheria ya Serikali za Kaunti kiti cha gavana kikisalia wazi, uchaguzi mdogo unapasa kufanywa ndani ya siku 60. Hii ni ikiwa kiti cha naibu gavana pia kiko wazi ambapo kwa wakati huu Spika wa Bunge la Kaunti ndiye atatekeleza majukumu ya Gavana wa kaunti husika.

Ikiwa Seneti itaidhinisha hoja ya kutimuliwa afisini kwa Bw Sonko, hii ina maana kuwa uchaguzi mdogo wa ugavana wa Nairobi utafanyika mwishoni mwa Februari 2021.

Shughuli hiyo itafanyika miezi miwili kabla ya kura ya maamuzi ya kuidhinisha marekebisho ya Katiba yaliyopendekezwa na mswada wa BBI. Kura hiyo ya maamuzi imeratibiwa kufanyika mwishoni mwa Aprili, kulingana na mpangilio wa Sekritarieti inayoongoza shughuli hiyo.

Hoja ya kumwondoa afisini Bw Sonko ilipitishwa Alhamisi wiki jana baada ya kuungwa mkono na madiwani 88 kati ta 122 wa bunge la kaunti ya Nairobi. Hoja hiyo ilidhaminiwa na kiongozi wa wachache Michael Ogada.

Wengi wa madiwani walipiga kura kwa njia ya mtandaoni wakati wa kikao baada ya mjadala kuhusu hoja hiyo. Ni madiwani wawili pekee walipinga hoja hiyo.

Kulingana na hoja hiyo, Bw Sonko aliondolewa mamlakani kwa matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, mienendo mibaya, kudinda kuidhinisha bajeti iliyotengewa Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) ya Sh27.7 bilioni na kutokuwa na uwezo kimwili na kiakili kuendesha shughuli za serikali ya kaunti hiyo.