Michezo

Baadhi ya vijana wa Angaza Youth wazuru Ufaransa kupitia ufadhili

August 6th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WASICHANA watatu na wavulana wawili wa timu ya Angaza Youth Team yenye mizizi yake Kiandutu, Thika, walizuru Ufaransa kwa ufadhili wa mashirika mawili ya ng’ambo.

Mashirika hayo; Street Football World na Sports Dans La Ville ya Ufaransa, yanalenga kuboresha hali ya maisha ya vijana kote ulimwenguni.

Mashirika hayo yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakiwafadhili vijana chipukizi wenye vipaji na umahiri katika michezo, sanaa na maswala ya kitamaduni.

Kiongozi wa msafara wa timu ya Angaza Youth Team, Zacharia Ochola alisema ziara hiyo ya Julai 2019 ilichukua muda wa wiki moja katika mji wa Lyon nchini Ufaransa.

“Vijana hao wamepata hamasisho tosha kuhusu maswala ya soka, sanaa, na utamaduni. Na lengo kuu la ziara hiyo ni kuona ya kwamba vijana kutoka nchi kadha ulimwenguni zinakongamana kwa lengo kuu la kubadilishana mawazo kwa kusoma tamaduni tofauti za nchi hizo,” alisema Ochola.

Alisema nchi 35 ziliwakilishwa, baadhi zikiwa ni Ufaransa, Ujerumani, DR Congo, Uingereza, Ubelgiji na Kenya.

Kikosi cha Angaza Youth, kilikuwa cha vijana wasiozidi umri wa miaka 18 ambapo wasichana waliwakilishwa na Pauline Nanjala (Archivers High), Carolyne Waithera (kinara wa wasichana hao), na Phoebi Fwanga (High View Sec).

Wavulana waliwakilishwa na Edwin Macharia (Broadway Secondary), na Emmanuel Okubasu (M-Pesa Foundation Academy).

Kuboresha ujuzi

Ochola alisema lengo kuu la kuwaleta vijana chipukizi pamoja ni kuboresha ujuzi wao wa soka, kuwapa mwelekeo wa kujitegemea kimaisha na jinsi ya kujieleza mbele ya umati.

Vijana wote walioshiriki walikabidhiwa medali kuthibitisha kushiriki kwao katika kongamano hilo.

Alisema mashirika hayo yamekuwa yakifadhili Angaza Youth kama shirika linalojumuisha maswala kadha katika jamii.

Aliongeza kwamba Angaza inafunza vijana kuhusu teknolojia kwa kutumia vipatakilishi na pia kueneza soka katika mitaa duni kama Kiandutu, Kiang’ombe na Umoja, mjini Thika na vitongoji vyake.

Wakati vijana wa Angaza Youth Team walizuru Ufaransa walipata fursa ya kushuhudia mechi za nusu-fainali za Kombe la Dunia upande wa Wanawake zilizopigiwa uwanjani Groupoma nchini Ufaransa.

Kila mwaka vijana wengi kutoka nchi tofauti hupata fursa ya kipekee kuzuru nchi ya Ufaransa kwa udhamini wa mashirika hayo mawili.

Alisema shirika hilo limesema litazidi kushirikiana na Angaza Youth Team pamoja na maafisa wake wakuu ili kuona ya kwamba kila mara wanawafadhili vijana wachache kuzuru Ufaransa.

“Kitu muhimu tunachohimiza katika kikosi hicho cha vijana ni maswala ya nidhamu. Kabla kusajili kijana yeyote ni sharti tuzungumze kwa kina na wazazi wake au walezi,” alisema Ochola ambaye pia ni mmoja wa maafisa wakuu katika kikundi hicho cha Angaza Youth Team.