Habari

Baadhi ya wabunge watetea Matiang'i na Kibicho

November 14th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa ‘Kieleweke’ wamemtaka Niabu Rais William Ruto kukubali kushindwa kwa mgombea wa chama hicho McDonald Mariga huku wakimtaka akome kuingiza jina la Waziri wa Usalama Fred Matiang’i katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra.

Huku wakiandamana na wenzao wa ODM, walitaja madai ya wabunge wanaounga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022, kwamba Dkt Matiang’ i, katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho na kiongozi wa ODM Raila Odinga walikutakana katika hoteli moja kupanga fujo, kama yasiyo na ukweli wowote.

“Tunajua hii ni njama ya kundi la ‘Tangatanga’ kuwaharibia jina Waziri Matiang’i, Dkt Kibicho, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na watumishi wengine wa umma ili ionekane kwamba Naibu Rais analengwa na serikali,” akasema Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu katika Bunge la Kitaifa Gathoni Wa Muchomba kwenye kikao na wanahabari Jumatano katika majengo ya bunge, Nairobi.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu katika Bunge la Kitaifa Gathoni Wa Muchomba (wa pili mbele kushoto) kwenye kikao na wanahabari Jumatano, Novemba 13, 2019, katika majengo ya bunge, Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

Alisema Dkt Ruto na wabunge wandani wake wanatafuta kisingizio cha kupinga ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) “baada ya kushindwa katika uchaguzi mdogo wa Kibra”.

“Tungependa kumshauri Naibu Rais na wenzake wakubali kuwa walishindwa katika uchaguzi wa Kibra na wakome kuwalaumu watumishi wa umma ambao hawakuhusika kwa njia yoyote katika uchaguzi. Na wajue kwamba tutawashinda tena ripoti hiyo itakapowasilishwa bungeni,” akasema Bi Wa Muchomba.

Vilevile, walipinga madai kwamba Bw Odinga anahujumu BBI wakiyataja kama “porojo ambazo hazina msingi wowote.”

Naye Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu aliwaomba wenzao wa tangatanga kukoma kumshambulia Waziri Matiang’I na Dkt Kibicho ambao hawakuhusika katika kampeni za Kibra.

“Ikiwa walipata habari kuhusu mkutano ambao Matiang’i alifanya kujadili uchaguzi mdogo wa Kibra, mbona hawakutoa habari hizo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na asasi zingine huru?” akauliza Bw Wambugu.

Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi na mwenzake wa Borabu Ben Momanyi walimsuta mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa kufuatia madai yake kwamba Dkt Matiang’i alishirikiana na Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati kupanga fujo zilizoshuhudiwa Kibra.

“Matamshi hayo ya Ichung’wa yanaiharibia sifa jamii yetu ya Wakisii. Sisi kama jamii ni watu wapenda amani na kamwe hatuwezi kushiriki uhalifu. Madai haya ni matusi kwetu kama jamii,” akasema Bw Angwenyi.

Madai mazito

Mnamo Jumanne Bw Ichung’wa na wenzake walidai kuwa siku moja kabla ya siku ya uchaguzi mdogo wa Kibra Dkt Matiang’i na Kibicho walikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupanga njama ghasia hizo.

“Tuna habari kwamba Odinga, Matiang’i na Kibicho walikutana katika hoteli moja mtaani Karen kupanga namna ambavyo wangetumia magenge ya wahalifu kusababisha fujo katika uchaguzi huo. Kwa hivyo, sasa tunajua kuwa magenge ya wahalifu waliowavamia wabunge Kibra yalikuwa na ulinzi kutoka kwa watu wanaohudumu katika ofisi ya Rais,” Bw Ichungwa akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Mbunge huyo alikuwa ameandama na wenzake; Caleb Kositany (Soy), David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki), Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Karatina), Japhet Mutai (Bureti), Kagongo Bowen (Marakwet Mashariki), Jayne Kihara (Naivasha) miongoni mwa wengine.

Hata hivyo, wabunge hao hawakutoa ithibati yoyote kuhimili madai yao huku wakisema hawawezi kuandikisha taarifa kwa polisi kwa sababu “hatua hiyo haina maana yoyote.”

Hata hivyo Jumatano, wenzao wa ‘Kieleweke’ waliwashauri kuwasilisha malalamishi yao katika kituo chochote cha polisi “ikiwa wanahisi walikosewa”.