Baadhi ya wakazi wa Thika washerehekea baada ya Karua kutangazwa mgombea mwenza wa Raila

Baadhi ya wakazi wa Thika washerehekea baada ya Karua kutangazwa mgombea mwenza wa Raila

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa mji wa Thika walijitokeza barabarani Jumatatu wakishangilia baada ya kinara wa Azimio Raila Odinga kumteua Martha Karua awe mgombea mwenza wake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Baadhi ya wakazi waliambia Taifa Leo tiketi ya wawili hao ni bora zaidi katika kupambana na ufisadi na kusuluhisha matatizo mengine yanayokumba nchi.

Bi Mary Kirika anayewania kiti cha ubunge Thika alisifu hatua hiyo kwa kusema ya kwamba “tutaona mwamko mpya katika nchi yetu.”

“Hatua hiyo ni mojawapo ya hatua muhimu alizochukua Bw Odinga na kwa hivyo ni heshima kubwa kwa wanawake wa nchi yetu,” alieleza Bi Kirika.

Alisema ana imani kuwa muungano huo utaleta mvuto na hatimaye ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Sisi kama wanawake tunastahili kuungana kama kitu kimoja kuona ya kwamba mwenzetu Bi Karua anaingia katika uongozi wa juu hapa nchini. Tutafanya juhudi kuona ya kwamba tikiti ya Raila na Karua inaingia ikulu,” alisema Bi Kirika.

Alisema ana imani Bw Odinga atahakikisha uongozi unaafiki uwakilishi jinsia unaohitajika kikatiba.

Kulingana na Bw Odinga ni kwamba Bi Karua atapewa jukumu la kuwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Kikatiba ili kupambana na maswala tata ya ufisadi na uhalifu nchini.

Bw Simon Kariuki mkazi wa Thika alikaribisha hatua ya Bw Odinga kumteua Bi Karua kuwa naibu wake kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Tayari Bw Odinga ameonyesha jinsi anavyojali maslahi ya wanawake hapa nchini. Kwa hivyo Wakenya wanastahili kumuunga mkono,” alisema Bw Kariuki.

Naye Bi Jane Wairimu, alisema hatua hiyo ni heshima kubwa kwa wanawake ambapo wataweza kutambulika hapa nchini na hata ulimwenguni.

“Sisi kama wanawake tunastahili kumshika mkono dada yetu Bi Karua ili tuweze kutambulika na kupata heshima inayostahili,” alisema Bi Wairimu.

Alisema Kenya imeanza kuchukua mwelekeo mpya ambao una tija ulimwenguni kote.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa Kangemi Allstars asema heri kuvuna alama moja...

Rigathi Gachagua aahidi kuwaambia wakazi wa Mathira...

T L