Makala

Baadhi ya waliofaidi kutokana na utawala wa Moi

February 5th, 2020 4 min read

Na CHARLES WASONGA

KATIKA utawala wa Rais mstaafu Daniel Moi kuna watu kadhaa ambao walifaidika pakubwa kwa kuwa wandani wake katika nyanja za biashara, siasa na serikalini.

Tunaelezea wasifu wa baadhi yao katika makala hii.

HEZEKIAH OYUGI

Marehemu Hezekiah Oyugi anakumbukwa kama afisa wa serikali aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika utawala wa Rais mstaafu Moi, haswa alipohudumu kama Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani. Hii ilitokana na uamunifu wake kwa Rais huyo.

Katibu huyo zaidi na maafisa wa utawala wa mkoa kiasi kwamba baadhi yao wangesimama na kupiga saluti wakiongea naye kwenye simu, hata kama Oyugi alikuwa akipiga simu kutoka Nairobi.

Pia anakumbukwa kupambana vikali na watu waliodhaniwa kwa waasi wa serikali katika miaka ya 1980s. Bw Oyugi aliondolewa kwa wadhifa huo mnamo Oktoba 1991 baada ya kuhusishwa na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni Robert Ouko.

JOSHUA KULEI

Bw Kulei ambaye aliwahi kuhudumu kama karani wa Rais Mstaafu Moi ni miongoni mwa watu tajiri zaidi nchini Kenya kulingana na jarida la Forbes. Baadhi ya mali hizo anamilika pamoja na familia ya Moi, mfano kundi la kampuni kwa jina, Sovereign Group, linalomiliki asimilia 33 katika mkahawa wa Intercontinental Hotel. Hata hivyo, Kulei anakabiliwa na kesi kadha za ufisadi kortini.

HOSEA KIPLAGAT

Hosea Kiplagat ni mfanyabiashara na mwanasiasa ambaye alifaidi pakubwa kutokana na uhusiano wake wa karibu na Rais mstaafu Daniel Moi.

Ni uhusiano huu uliomwezesha kupanda ngazi kutoka kazi ya askari jela hadi akawateuliwa kuwa mwenyekiti mtendaji wa Kanu, tawi la Baringo. Ni tawi la hilo pekee nchini ambalo lilikuwa na cheo kama hicho.

Wakati wa utawala wa Moi, Bw Kiplagat pia aliweza kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Cooperative, cheo kilichomwezesha kuwa na ushawishi mkubwa katika sekta ya biashara.

Hata hivyo, mnamo 2007 Kiplagat aliwania kiti cha ubunge cha Baringo ya Kati lakini akaangushwa na Sammy Mwaita.

SHARIFF NASSIR

Alifaidi pakubwa, kisiasa na kibiashara, kutokana na uhusiano wake wa karibu na Rais Moi.

Hii ilitokana na hali kwamba marehemu Nassir alikuwa mfuasi na mtetezi sugu wa KANU katika iliyokuwa Wilaya ya Mombasa.

Alishikilia cheo cha mwenyekiti tawi la Mombasa kuanzia mwaka wa 1972. Na mnamo mwaka wa 1974, alitumia ushawishi huo kushinda kiti cha ubunge cha Mvita, alichokishikilia hadi mwaka wa 2002.

WILLIAM ODONGO OMAMO

Alikuwa mwandani mkubwa wa Moi katika Wilaya ya Siaya na ambaye Moi alimtumia kumpiga vita aliyekuwa hasidi wake mkuu eneo hilo, na kitaifa, Jaramogi Oginga Odinga.

Mnamo 1981 wakati ambapo aliyekuwa Mbunge Hezekiah Ougo alijiuzulu ili atoe nafasi kwa Jaramogi kuingia bungeni kupitia uchaguzi mdogo, Kanu ilimzuia Jaramogi kushiriki uchaguzi huo.

Hatua hiyo ilisababisha Omamo kushinda katika uchaguzi huo mdogo na hatimaye akateuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.

NICHOLAS BIWOTT

Nicholas Biwott ni mwanasiasa ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa zaidi alipohudumu katika serikali ya Rais Moi kama Waziri katika nyadhifa mbalimbali.

Alipewa lakabu ‘Total Man’ kuashiria ushawishi aliokuwa nao katika utawala wa chama cha Kanu, hasa katika ngome ya Moi ya Rift Valley.

Uhusiano wa karibu kati ya Moi na Biwott ulianza mnamo 1971 wakati ambapo Rais huyo wa pili alihudumu kama Makamu wa Rais. Biwott aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mnamo 1979 baada ya kushinda kiti cha Keiyo Kusini. Hapo ndipo ushawishi wake katika utawala wa Moi alianza kukita kwa kutunukiwa nyadhifa mbalimbali za uwaziri. Baadhi ya wizara hizo ni; Kawi, Viwanda, Kilimo na Biashara.

Sawa na wanasiasa wengine wa Kanu nyakati hizo uhusiano huu ulimwezesha Biwott kujilimbikizia mali nyingi.

KARIUKI CHOTARA

Alikuwa mwandani mkubwa wa Moi katika Wilaya ya Nakuru ambaye anakumbukwa kwa kuanzisha kundi la vijana wa Kanu (Kanu Youth Wing) kuvumisha chama hicho.

Chotara alitwaa wadhifa wa mwenyekiti wa Kanu Wilayani Nakuru mnamo 1979 baada ya Moi kukosana na Kihika Kimani ambaye ni mmoja wa wanasiasa waliounda vuguvugu la kupigania mabadiliko ya Katiba ili kumzuia kumrithi Rais Kenyatta.

Kundi hilo la vijana wa Kanu liliogopewa zaidi hata kuliko maafisa wa polisi kwa sababu wanachama walipenda kufanya operesheni kadha katika miji ya Nakuru na Naivasha kuwakamata washukiwa wa “makosa madogo”.

Bw Chotara alishirikisha shughuli za Kanu katika wilayani Nakuru na alipambana na wale waliodhaniwa kuwa maadui wa Kanu. Na sasa na wanasiasa wengine, alitumia nafasi hiyo kujilimbikizia mali nyingi. Chotara, alifariki mnamo Januari 9, 2019.

JACKSON ANGAINE

Katika eneo zima la Meru marehemu Jackson “Harvester” Angaine ni mmoja wa wanasiasa ambao walifaidi katika utawala wa Rais Mstaafu marehemu Daniel Moi.

Alihudumu kama mwenyekiti wa KANU katika iliyokuwa wilaya ya Meru kuanzia mwaka wa 1963 alipohudumu kama mbunge wa Imenti Kaskazini na Waziri wa Ardhi katika utawala wa Rais wa kwanza Jomo Kenyatta.

Mnamo 1983, chini ya Utawala wa Rais Moi, Bw Angaine, ambaye alifariki mnamo 1999, aliteuliwa serikali kuwa Waziri katika Afisi ya Rais, wadhifa ambao alishikilia hadi 1992 aliposhindwa na David Mwiraria katika uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Marehemu Angaine alikuwa sikio na macho ya Mzee Moi na utawala wa Kanu katika eneo lote Meru.

MULU MUTISYA

Japo hakuwa amesoma, marehemu Mulu Mutisya aliheshimia kama “Baba wa Siasa za Ukamba” wakati wa utawala wa Moi, kwa sababu alikuwa mwandani wake wa karibu.

Ni Bw Mutisya aliyemjulisha kigogo wa siasa Ukambani wakati huu Kalonzo Musyoka kwa Rais Moi na ndipo nyota yake ya kisiasa inaanza kung’aa.

Ucheshi wake uliweza kumfanya kupendwa na wengi, akiwemo Rais Moi. Kando na kushikilia wadhifa wa mwenyekiti wa Kanu, Mutisya aliweza kuteuliwa na Moi bodi ya shirika la uhifadhi wa mazingira.

EZEKIEL BARNG’ETUNY

Bw Barng’etuny ambaye alikuwa mfanyabiashara na mwanasiasa kutoka eneo la Nandi alifaidi katika serikali ya Rais Moi kutokana na weledi wake katika udalali. Kila mwaka angeandama na Moi katika mnada wa katika eneo la Kimalel, kaunti ya Baringo. Kwa sababu hii, Bw Barngetuny alifanikiwa kuteuliwa kuwa Mbunge Maalum katika miaka ya 1980s na 1990s.

MARK TOO

Maarufu katika ulingo wa siasa kama ‘Bw Dawa’ au kwa kimombo ‘Mr Fix It’ kutokana na weledi wake katika usuluhishaji mambo, Bw Too alifaidi pakubwa kutokana na uhusiano wake na Mzee Moi.

Nyota yake iling’aa katika ulingo wa biashara baada ya Moi kumsaidia kufahamiana na aliyekuwa mwanzilishi wa kampuni ya Lonrho Group Roland “Tiny” Rowland.

Baadaye Bw Too alishikilia wadhifa wa mwenyekiti wa kampuni hiyo ilipoitwa Lonrho East Africa. Baada ya uchaguzi mkuu wa 1997, Rais Moi alimteua kuwa Mbunge Maalum. Lakini alihudumu kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kumshawishi ampishe Rais Uhuru Kenyatta.

Watu wengine waliofaidi kutoka na uhusiano wao wa katibu na Moi ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha KANU J. J Kamotho, aliyekuwa Waziri wa Elimu Peter Oloo Aringo, miongoni mwa wengine wengi.