Baadhi ya wanafunzi wafanyia KCSE hospitalini, jela

Baadhi ya wanafunzi wafanyia KCSE hospitalini, jela

KALUME KAZUNGU NA SIAGO CECE

WATAHINIWA wawili wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) katika Kaunti ya Lamu, walilazimika kufanya mitihani hiyo iliyoanza Jumatatu hospitalini baada ya kujifungua.

Katika Kaunti ya Kwale, watahiniwa watano waliokuwa kizuizini wakikabiliwa na madai ya kuchoma shule zao mwaka uliopita, walipata afueni baada ya kuachiliwa kwa dhamana.

Mtahiniwa mmoja ndiye angali kizuizini ambapo alipelekewa mitihani yake.Wanafunzi waliojifungua Lamu ni wa kutoka shule za upili zilizo maeneo ya Witu na Mpeketoni.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Lamu, Bw Joshua Kaaga, alisema mmoja alikuwa amejifungua Jumamosi ilhali mwingine akijifungua Jumapili usiku.

Bw Kaaga alisema Wizara ya Elimu ilikuwa imetekeleza maandalizi ya mapema kwa wasichana hao kufanya KCSE hospitalini kwani siku zao za kujifungua zilikuwa zimewadia.

Alisema mbali na vituo 26 vya KCSE vilivyoko Lamu, hospitali walimojifungulia pia iliongezwa kuwa kituo cha 27.

Jumla ya watahiniwa 1,828 wanaojumuisha wavulana 1,005 na wasichana 823 wanafanya mtihani huo Kaunti ya Lamu mwaka huu.

Katika Kaunti ya Kwale, mtahiniwa aliyedaiwa kuhusika katika uchomaji wa shule alianza mitihani yake akiwa katika gereza la wanawake la Kwale.

“Mtahiniwa mmoja bado yuko jela na anaendelea na urekebishaji wa tabia kwa sababu alihusika katika uchomaji wa shule,” akasema Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Kwale, Bw Martin Cheruiyot.

Watahiniwa 8,989 watafanya mitihani yao ya kitaifa katika Kaunti ya Kwale kwa muda wa wiki tatu zijazo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, maafisa wanaosimamia mitihani hiyo walishikwa na wasiwasi baada ya kasha la mitihani kuonekana limetoboka.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Kwale, Bw Ambrose-Steve Oloo, alisema hapakuwa na haja ya kutia shaka kwani maafisa kutoka Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC) waliitwa na kuthibitisha kuwa mitihani yote ilikuwa sawa.

“Tunadhani ni shimo lililotokana na masanduku hayo kusafirishwa kutoka Nairobi hadi Kwale. Hakuna mitihani iliyoibwa,” Bw Oloo alisema.

Mwaka huu, jumla ya watahiniwa 831,015 walisajiliwa kufanya mtihani huo kitaifa katika vituo 10,413.

Idadi hiyo ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo watahiniwa 752,981 walifanya KCSE.

You can share this post!

JIJUE DADA: Jinsi ya kuhesabu mzunguko wako wa hedhi...

Ni kufa-kupona Utd, Atletico leo

T L