Makala

Baadhi ya wanahisa Embakasi Ranching wapendekeza mbinu iliyotumika Kihiu Mwiri

August 6th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

KUNDI moja la wanahisa katika mradi wa ununuzi na uuzaji mashamba wa Embakasi Ranching sasa linamtaka Rais Uhuru Kenyatta aagize marufuku ya kampuni hiyo kama ya kibinafsi.

Kundi hilo likiongozwa na msemaji wa wanaopambana wanahisa watuzwe hatimiliki bila masharti, Bi Miriam Wanjiku limesema kumekuwa na ule limeita ni mchezo wa paka na panya katika mradi huo, hali ambayo inasambaratisha uwezekano wa hati kupatikana.

Rais Kenyatta alikuwa ametangaza nia ya serikali ya kuvunjilia mbali kampuni hiyo ambayo ina miaka 44 hadi sasa na kisha serikali itoe hatimiliki kabla ya Februari 1, 2018.

Hata hivyo, hadi sasa, afisi ya Rais imekuwa ikiahirisha shughuli hiyo kila mara kwa mara zote tano ambazo imepania kufanya hivyo tangu wakati huo kwa msingi wa malumbano ya kiuongozi.

Hadi sasa, kuna kambi mbili za uongozi ambazo zinang’ang’ania mamlaka ya kuwa bodi ya ukurugenzi katika kampuni hiyo, hali ambayo inazidisha ugumu wa wanahisa kupata hatimiliki.

Kwa mujibu wa mmoja wa anayetambuliwa kama mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo, Bi Leah Mathenge “ni ukweli kuwa kumekuwa na shida ya uongozi hapa ambapo kuna baadhi ambao kupitia njia za mkato wamejipa hati ya uongozi ilhali kuna utaratibu wa kunibadilisha kama kiongozi.”

Kwa upande wake, anayeongoza mrengo wa kutimua Bi Mathenge mamlakani akifahamika kama John Mingi Njoroge anasema uongozi wa Bi Mathenge hautambuliki kwa kuwa haukuidhinishwa na wanahisa katika mkutano wa kila mwaka (AGM).

Anasema kuwa Bi Mathenge alikuwa afisini kama kaimu mwenyekiti baada ya kuingia mamlakani baada ya kifo cha Bw Mwangi Thuita ambaye kwa muda mrefu alikuwa mwenyekiti. Alifariki mwaka 2018.

“Sisi tuliandaa mkutano huo wa AGM mnamo Juni 13 katika jumba la KICC na nikaidhinishwa kuwa mwenyekiti na ambapo kwa sasa ninapinga harakati zilizoko za kutoa hati miliki hadi wakati ule tutaandaa orodha ya wanahisa kamili na tung’oe matapeli ambapo wamepenyezwa katika orodha inayoswemwa itatumika kutoa hati hizo,” anasema Bi Mathenge.

Anadai mrengo wa Bi Mathenge umeshirikiana na matapeli katika afisi ya Naibu Waziri wa Ardh Gideon Mung’aro kuunda orodha iliyo na shaka na ambapo ikitumika kutoa hati hizo, “kuna ukora mkuu utahalalishwa ndani ya mradi huu.”

Bi Wanjiku anamtaka Rais pamoja na maafisa wengine waingilie kati na wazime mgogoro huu wa uongozi ili harakati za kutoa hatimiliki zifanikishwe.

“Kila wakati tunafikiria tumepiga hatua, tunajipata tumekwama katika mzozo wa kiuongozi. Serikali kupitia Rais ina uwezo wa kutupokonya leseni ya usajili kama kampuni ya kibinafsi. Serikali ndiyo mamlaka kuu ya kuhalalisha kampuni hapa nchini na kwa kuwa inapania kuvunja na kutoa hatimiliki ili wanahisa wakajijenge na vipande vyao vya ardhi. Mwanzo ni tupokonywe leseni ya usajili,” akasema.

Kihiu Mwiri

Bi Wanjiku aliswema kuwa njia kama hiyo ndiyo ilitumika katika mradi wa Kihiu Mwiri ambao baada ya serikali kujaribu mara kadhaa kutoa hatimiliki na kulemewa kupitia njama za mauaji kati ya waliokuwa wakiing’ang’ania, Rais aliamrisha mradi huo uvunjwe kupitia kupokonywa leseni ya usajili.

Hali hiyo ndiyo mrengo wa Bi Wanjiku unapendekeza itekelezwe kwa Embakasi Ranching.

Miaka ya sitini (1960s), marehemu Njenga Karume aliungana na mwanzilishi wa taifa Mzee Jomo Kenyatta na mwanasiasa Muhuri Muchiri kuzindua mradi huo.

Mradi huo uliambatana na mingine mingi ambayo iliwasaidia baadhi ya watu kutoka eneo la Kati kupata mashamba katika maeneo mengine nchini hasa Rift Valley na Pwani.

Hata ikiwa kuna tetesi kuwa baadaye Karume alianza kuuza baadhi ya mashamba hayo kwa serikali hasa ya Rais Mwai Kibaki, hivyo basi kujipatia faida kubwa, wengi wa walionufaika leo hii hutambua juhudi zake kama zilivyowawezesha kuekeza katika ardhi.

Mwanzoni, mradi huo wa Embakasi ulikuwa ukijihusisha na uzalishaji wa mboga na matunda, ukapanua shughuli zake hadi uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa na hatimaye hisa zake zikaanza kuuzwa kwa watu maskini.

Hisa hizo zilikuwa Sh40 ili mwanahisa ajipatia robo ekari ya kipande cha ardhi katika maeneo ya Embakasi, Kitengela na Syokimau.

Mnamo miaka ya thamanini (1980s), mradi huo ulikuwa umepanuka hadi kuwa na hekari 13,500 ambazo zinadhibitiwa na wanahisa 5,500.