Habari Mseto

Baba ajiua baada ya kukosana na mwanawe

February 13th, 2018 1 min read

Na GERALD BWISA

MWANAMUME wa miaka 55 Jumatatu alijiua baada ya kugombana na mwanawe katika kaunti ya Trans Nzoia.

Marehemu, aliyetambuliwa kama Patrick Kimamo, anadaiwa kujinyonga mwendo wa saa 11 alfajiri katika kijiji cha Kibomet, katika kata ndogo ya Naisambu.

Inadaiwa kwamba mwathiriwa alichukua hatua hiyo baada ya kugombana na mwanawe kwa kuuza mojawapo ya magari yake bila kumwambia.

Mkewe wa pili, Jentrix Chepkemoi, aliiambia Taifa Leo kwamba baadaye gari hilo lilisababisha ajali, ambapo mwathiriwa alitaka kulipwa ridhaa.

Bi Chepkemei aliongeza kwamba mwanawe amekuwa akifuja pesa alizokuwa akipewa na marehemu kumpelekea katika benki.

Alisema kwamba mumewe aliamka mwendo wa saa 10 alfajiri, ambapo alidai kwamba alikuwa akienda kunyunyizia mboga maji.

“Haikuwa kawaida yake kuamka mapema kiasi hicho. Hivyo, niliamka baada ya dakika 15, ambapo nilimpata akiwa ananing’inia katika chumba cha nguruwe. Alikuwa amejifunga shingoni kwa kamba,” akasema.

Mkuu wa Polisi wa Trans Nzoia Magharibi, Jackson Mwenga, alithibitisha kisa hicho, akisema kuwa wanatuhumu kiini kikuu kuwa mzozo wa kinyumbani.

Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Kitale