Kimataifa

Baba amng'ata mamba mguu kuokoa mwanawe

January 31st, 2019 1 min read

MAHIRIKA Na PETER MBURU

BABA mmoja kutoka Ufilipino Alimwokoa mwanawe wa kiume kutoka mdomo wa mamba kwa kumuuma mnyama huyo mguuni hadi akamwachilia mtoto wake.

Iliripotiwa kuwa Diego Abulhasan, mtoto wa miaka 12 alikuwa akiogelea pamoja na kakake mchanga katika mto ulio karibu na nyumbani kwao mji wa Balabac, eneo la Palawan, wakati mamba alimvamia na kumvuta majini.

Baba yao alisikia mayowe ya wanawe wakiitisha msaada na akakimbia upesi umbali wa kama mita 100 kutoka boma lilipo, kisha akaruka mtoni akiwa amejihami na kuni.

Bw Abulhasan alianza kumchapa mnyama huyo kwa kuni na ngumi lakini hakumwachilia mwanawe. Alipoona mambo yanaharibika, alimkamata mnyama huyo na kumuuma mguuni mara kadha hadi akamwachilia mtoto na kuogelea akitoroka ndani ya maji kabisa.

Baadaye baba huyo alimchukua mwanawe na kumtoa majini kisha akamkimbiza hospitalini. Bw Abulhasan alieleza umma kuwa hangeweza kusita kujirusha ndani ya maji kupigana na mamba huyo alipoona hata aliyokumbana nayo mtoto wake.

“Sikuwa na wakati wa kuwaza. Nilikuwa nikimchapa mamba na hakumwachilia mtoto wangu. Tulipigana na mamba huyo hadi tukaangaliana macho kwa macho. Kisha mara moja wazo likanijia nimuume, nilishika mguu wake mara moja na kuuuma kwa nguvu kabisa kama mbwa,” akasema baba huyo.

Mtoto huyo alilazwa hospitalini kwa siku mbili kisha akaruhusiwa kwenda nyumbani. Alipata alama kadha, japo hakujeruhiwa vibaya.

Polisi walisema kuwa ni kutokana na ushujaa wa babake mtoto huyo ndipo hakuuawa na mnyama huyo, wala kujeruhiwa vibaya.