Habari MsetoKimataifaSiasa

'Baba' apewa mlinzi rasmi wa serikali nchini Ghana

September 13th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa upinzani Rais Odinga alitunukiwa hadhi na heshima ya kipekee nchini Ghana Alhamisi kwa kupewa mlinzi rasmi wa serikali (ADC) alipotua huko kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Kofi Annan.

Kwenye picha alizoweka katika ukurasa wake wa Facebook, Bw Odinga anaokana akitoa heshima zake za mwisho kwa mwendazake Annan huku nyuma yake akisimama afisa wa cheo cha juu jeshini. Afisa huyo, aliyevalia mavazi rasmi, anaonekana akimfuata unyo unyo hata baada ya kutoa heshima zake.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Odinga kupewa hadhi ya kiwango hicho anapozuru taifa la kigeni tangu alipozika tofauti za kisiasa baina yake na Rais Uhuru Kenyatta Machi 9 mwaka huu.

Isitoshe, duru kutoka Wizara ya Mashauri ya Kigeni zinasema kuwa mabalozi wa Kenya katika mataifa yote ya Kigeni wameshauriwa kuwa wakimpokea rasmi Bw Odinga anapozuru mataifa wanakohudumu. Kiongozi huyo wa ODM pia hutumia magari ya ubalozi wa Kenya katika mataifa ya kigeni, kando na huduma nyinginezo.

Ujumbe wa Kenya katika mazishi ya Dkt Annan pia ulijumuisha Spika wa Seneti Kenneth Lusaka, ambaye alimwakilisha Rais Uhuru Kenyatta, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na Mbunge Mwakilishi wa Murang’a Sabina Chege.

Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga aandamana na mlinzi wake nchini Ghana. Picha/ Hisani

Pia alikuwepo dadake Bw Odinga, Ruth Odinga.

Marehemu Annan ambaye alifariki nchini Uswizi mwezi jana, alizikwa Alhamisi Septemba 13, 2018 kwa taadhima kuu katika makaburi ya kijeshi katika kitongoji cha Burma Camp jijini Accra, Ghana.

Annan anaenziwa na Wakenya kwa kuongoza juhudi za kurejesha amani nchini kufuatia ghasia za kisiasa zilizotokea nchini baada ya uchaguzi mkuu wa 2007. Jumla ya watu 1,300 walikufa, wengine 650,000 wakaachwa bila makao kando na mali ya thamani kubwa kuharibiwa.

Kwenye risala zake, Bw Odinga alimtaja marehemu Annan mwanadiplomasia ambaye daima atakumbukwa kote ulimwenguni kutokana na juhudi zake za kuleta amani katika mataifa mengi yaliyokumbwa na mizozo.

“Kama Wakenya daima hatutasahau wajibu aliotekeleza katika taifa wakati wa vita vya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007. Tunamshukuru kwa kufaulu kurejesha amani nchini mwetu mnamo Aprili 28, 2008,” Bw Odinga akasema.

Kando na Ghana, Bw Odinga amezuru mataifa kama vile Ujerumani, India, Zimbabwe, Afrika Kusini, Sudan Kusini kati ya mengine baada ya maridhiano kati yake na Rais Kenyatta. Amekuwa akipewa mapokezi ya taadhima kuu katika mataifa hayo.