Habari

Baba legeza kamba kuhusu BBI, arai Ruto

November 17th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

NAIBU Rais, Dkt William Ruto amemtaka Kiongozi wa ODM Raila Odinga alegeze msimamo kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Dkt Ruto alishikilia kwamba ripoti hiyo ina mapungufu mengi na wanaotaka ipitishwe jinsi ilivyo huenda wana malengo yao ya kibinafsi wakihadaa wananchi kwamba wanataka kuboresha taifa.

Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakipigia debe BBI huku Bw Odinga akisisitiza kuwa mchakato wa kukusanya saini milioni moja za raia utaanza rasmi wiki hii licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wanaotaka pawepo mazungumzo kwanza.

Hata hivyo, Dkt Ruto anasisitiza kuwa taifa litapoteza umoja wake iwapo wanasiasa watagawanyika katika mirengo ya ‘Ndiyo’ na ’La’ ilhali bado kuna muda wa kuhakikisha pande zote zinakubaliana kuhusu yaliyomo kwenye BBI.

“Wale ambao wanaendeleza mjadala wa kuunga mkono BBI hawafai kuwaeleza Wakenya kwamba hakuna muda wa kuifanyia marekebisho. Iwapo hatuwezi kuoanisha ripoti hiyo basi tutaishia kuwa na katiba mbovu yenye mianya mingi ya kisheria,” akasema Dkt Ruto.

Naibu Rais ameshikilia kwamba licha ya kamati ya BBI kuchukua muda wa miaka miwili kuiandaa, ripoti hiyo haiwezi kupigiwa kura jinsi ilivyo kutokana na masuala mengi ndani yake yanayokinzana.

“Iwapo nia kuu ya kukumbatia ripoti hii ni kutatua mgawanyiko ambao hushuhudiwa kila baada ya uchaguzi, basi kwa nini baadhi yetu hatutaki msimamo mmoja uchukuliwe kuhusu BBI kabla ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi?” akasaili Dkt Ruto, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa afisi yake.

Dkt Ruto alisema hayo katika makazi yake mtaani Karen alipokutana na madiwani wa Bunge la Wajir walioongozwa na Kiongozi wa Wengi, Mohamud Gabane na mwenzake wa wachache Abdi Hussein.

Aidha, alishikilia kuwa atawaongoza wafuasi wake kuunga BBI iwapo marekebisho yanayohimizwa na mashirika mbalimbali yatajumuishwa katika ripoti hiyo.

“Hakuna haja ya kuharakisha kupitisha ripoti yenye kasoro iwapo nia yetu ni nzuri kwa nchi hii. Iwapo BBI inalenga kuhakikisha kuna umoja, basi masuala yanayoibuliwa yanafaa kutiliwa manani,” akaongeza.

Mabw Gabane na Hussein nao waliahidi kuwa Bunge la Kaunti ya Wajir halitaunga mkono BBI iwapo yaliyomo ndani yake hayatatoa kipaumbele kwa mahitaji ya raia.

Kauli yao iliungwa mkono na Diwani wa wadi ya Waghberi Rashid Karshey aliyedai lengo la BBI ni kuwatengea baadhi ya wanasiasa nafasi za uongozi.

“Tutawaeleza watu wetu waikatae hadi masuala tuliyowasilisha yajumuishwe. Hatuwezi kusonga mbele kwa kuwatengea baadhi ya wanasiasa nafasi huku Wakenya wengi wakiendelea kuteseka,” akasema.

Pia Dkt Ruto alidai kuwa matukio ya sasa yanaonyesha kuna wanasiasa wanaotaka kutumia kura ya maoni kuhusu BBI kuendeleza ajenda zao za kisiasa za 2020.

“Wakenya hawafai washiriki mjadala wa BBI kwa sababu baadhi ya watu wanasukumwa na kusawiriwa kama wa mrengo wa ‘La’ ilhali tunaweza kujadiliana na kuafikiana?” akaeleza.

Vilevile alisisitiza kwamba uongozi wa nchi unafaa kuahirisha mjadala kuhusu BBI na ujikite katika kupambana na virusi vya corona ambavyo vimehasiri mno maisha ya wananchi nchini.