Habari Mseto

Baba, mjomba wakamatwa kwa kunajisi mtoto mwenye umri wa miaka minne

May 15th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

POLISI eneo la Ahero, Kaunti ya Kisumu wamemkamata mwanamume na kakake, kwa madai ya kumnajisi bintiye mwenye umri wa miaka minne.

Inasemekana kuwa baada ya kumtendea unyama huo, mwanamume huyo alimpeleka bintiye hospitalini na kuwahadaaa madaktari kuwa alikuwa amepata ajali ya barabarani.

Lakini uchunguzi wa kimatibabu ulionyesha kuwa mtoto huyo alinajisiwa, jambo ambalo liliwafanya wafanyakazi wa hospitali hiyo ya Kaunti Ndogo ya Ahero kuwaita polisi.

Bi Caren Omanga ambaye ni afisa wa afya katika jamii alisema kuwa polisi walimkamata mwanamume huyo wa miaka 40 (babake mtoto huyo), pamoja na kakake wa miaka 28, lakini wakawaachilia baadaye.

Hii, kulingana na Bi Omanga ni licha ya kuwa ushahidi wa watu na mtoto mwenyewe ulionyesha kuwa alinajisiwa na wawili hao.

Lakini OCPD wa Nyando Leonard Matete alisema kuwa washukiwa waliachiliwa kwa kuwa hakukuwa na mlalamishi.

Ni baada ya mamake mtoto huyo kuripoti malalmishi ndipo wawili hao walikamatwa tena na chembe chembe za kufanya uchunguzi wa kisayansi zikachukuliwa na kupelekwa katika maabara ya serikali Kisumu.

“Hatungeweza kuwazuilia washukiwa bila mlalamishi awali, lakini baada ya mamake mtoto kupiga ripoti sasa tumewazuilia,” akasema Bw Matete.

Alisema kuwa mtoto huyo alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Afisa huyo alisema kumekuwa na ongezeko la visa vya dhuluma za kingono, akisema kuwa wiki mbili zilizopita, genge lilimbaka ajuza wa miaka 80 katika eneo la Rabuor, kando na visa vingine viwili vilivyoripotiwa eneo la Awasi.