Habari Mseto

Baba na mwanawe mbaroni kwa kumng’oa meno polisi

February 4th, 2019 1 min read

Na GEORGE ODIWUOR

POLISI kutoka Homa Bay wamemkamata baba na mwanawe waliompiga afisa wa polisi kwa mawe hadi meno yake yakang’oka alipoenda kumkamata mshukiwa mwingine aliyehusishwa na mzozo wa shamba katika mtaa wa Ka Peter viungani mwa mji wa Homa Bay.

Boniface Oremo, 48 na mwanawe Collins Oremo, 22 walimvamia afisa huyo aliyekuwa ameandamana na maafisa wengine wawili kisha kumpiga kwa mawe wakilenga kuwazuia kuwakamata mshukiwa huyo.

Moja wa maafisa hao wa polisi alipoteza baadhi meno yake jiwe lilipopenya na kumpata vilivyo mdomoni.

Naibu Chifu wa Kata ya Asego Tom Ondiek alisema kwamba wawili hao walikamatwa wakiwa mafichoni katika mitaa mbalimbali mjini Homa Bay baada ya kupata taarifa kwamba walikuwa wakisakwa na polisi.

Kulingana na OCPD wa Homa Bay Sammy Koskey, afisa wa polisi aliyenyakwa anaendelea kupokea matibabu huku washukiwa hao wawili wakiendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Homa Bay.