Habari Mseto

Baba na mwanawe wa miaka 3 wauawa kwa risasi na majangili

February 22nd, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ONDIEKI

BABA na mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu jana waliuawa na watu wanaodaiwa kuwa majangili katika kijiji cha Lolmolog, Kaunti ya Samburu.

Wawili hao walipigwa risasi baada ya kijiji hicho kuvamiwa na majangili eneobunge la Samburu Magharibi mapema mnamo Jumanne asubuhi.

Kamanda wa Polisi wa Samburu ya Kati, John Mwai alisema majangili hao walilenga kuiba mifugo katika kijiji hicho.

Babake alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi huku mwana akifariki dunia hospitalini ambako alikuwa amekimbizwa kupokea matibabu.

Miili ya wawili hao iko katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Samburu ikisubiri kufanyiwa upasuaji wa maiti.

Kwa mujibu wa Bw Mwai, majangili hao walikuwa wameanza kuhepa na zaidi ya ng’ombe 150 lakini polisi wa akiba wakafika kwa wakati na kuwatimua. Polisi jana walikuwa bado wanawaandama majangili hao huku usalama ukiimarishwa sana eneo hilo.

“Tuko chonjo na oparesheni za kiusalama bado zinaendelea ili tuhakikishe kuwa kuna amani katika eneo hili. Hatutapumzika hadi tuwakamate washukiwa hao na pia tunawaomba wananchi watoe habari ambazo zinaweza kutusaidia kuwanyaka majangili hao,” akasema Bw Mwai.

Mkuu huyo aliwaomba wenyeji wasilipize kisasi na badala yake wawape maafisa wa usalama muda wa kuwasaka na kuwanyaka majangili hao.

Serikali imekuwa ikikabiliwa na wakati mgumu katika kuhakikisha kuna usalama eneo la Samburu Magharibi.