Baba ndani kwa madai ya kumchoma mwanawe

Baba ndani kwa madai ya kumchoma mwanawe

Na KNA

POLISI wa Narok Mashariki, Kaunti ya Narok, wamemkamata mwanamume, 35, kwa madai ya kumshambulia mwanawe wa kambo kwa kumchoma kwa upanga moto katika sehemu tofauti mwilini mwake.

Mshukiwa, aliyetambuliwa kama Robert Ombaga, anadaiwa kufanya kitendo hicho katika kijiji cha Lemuten Kojonga, eneo la Mosiro.

Mtoto huyo ana umri wa miaka saba.

Akithibitisha kisa hicho, Naibu Kamishna wa eneo hilo, Jared Okari alisema mshukiwa huyo anadaiwa kumfanyia mwanawe unyama huo tarehe tofauti mamake alipokuwa ameondoka nyumbani.

Hata hivyo, mwathiriwa aliokolewa Jumamosi na majirani, mshukiwa alipokuwa akimfanyia unyama huo. Ni baada ya tukio hilo ambapo waliarifu polisi.

Mtoto huyo anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Narok, huku mshukiwa akizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Ntulele.

Anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo Jumatatu kwa shtaka la kumshambulia mwanawe.

Katika kujitetea kwake, mshukiwa anadai kuwa mwathiriwa amekuwa akimwibia pesa na bidhaa nyingine, hali iliyomfanya kumchukulia hatua hiyo.

Hata hivyo, madai hayo bado hajayathibitishwa.

Kulingana na Sheria ya Watoto 2016, ni makosa kumshambulia ama kumtishia mtoto kwa namna yoyote ile.

Sheria hiyo vilevile inampa haki mtoto kukulia katika mazingira mazuri ili kuwa mtu anayewajibika katika jamii ukubwani mwake.

Kwingineko, polisi katika Kaunti ya Trans Nzoia, Ijumaa waliwakamata wavulana wawili wa shule ya msingi baada ya kurejea shuleni wakiwa walevi.

Wawili hao walikamatwa katika Shule ya Msingi ya Chepkoilel, Kaunti Ndogo ya Saboti. Baadaye walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Sango ili kuhojiwa.

Duru katika shule hiyo zilisema kuwa wanafunzi hao wawili ni miongoni mwa wanafunzi kadhaa (wavulana na wasichana) ambao walirejea shuleni wakiwa walevi.

Wawili hao wako katika darasa la sita na saba mtawalia.

Wasimamizi wa shule hiyo waliripoti kisa hicho wa chifu wa Kata ya Kinyoro, Bi Rose Chebet, aliyewaongoza maafisa wa usalama kuwakamata wanafunzi hao wawili.

Hata hivyo, wanafunzi wengine walifanikiwa kukwepa kukamatwa kwa kutoroka shuleni.

Bi Chebet alisema wanafunzi hao wawili waliwapeleka polisi katika eneo ambako walimpata mwanamke anayedaiwa kuwauzia kileo hicho.

Polisi walifanikiwa kumkamata mshukiwa.

Kando na pombe, anadaiwa kuwauzia wanafunzi hao bangi.

  • Tags

You can share this post!

Ngilu ahimiza Kalonzo amuunge Raila mkono

Kiunjuri ashauri Ruto ashirikiane na vyama vingine