HabariSiasa

Baba Yao alivyotolewa pumzi

May 24th, 2019 2 min read

BENSON MATHEKA, ERIC WAINAINA na MARY WAMBUI

GAVANA wa Kiambu, Ferdinand Waititu Baba Yao, Alhamisi alikamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusiana na madai ya kuiba mamilioni ya pesa za umma.

Aliachiliwa baadaye jioni baada ya Hakimu Mkuu wa Kiambu, Brian Khaemba kumpatia dhamana ya kuzuia kukamatwa ya Sh500,000.

Bw Waititu alikamatwa saa chache baada ya mwenzake wa Murang’a, Mwangi wa Iria, kuhojiwa na maafisa wa EACC kuhusu shamba alilodaiwa kununua eneo la Kabati kwa bei ya Sh390 milioni.

Wapelelezi wanasema bei ya shamba hilo la ekari 10 ni ya juu mno kuliko ile ya kawaida. Bw Wa Iria aliruhusiwa kwenda nyumbani mwendo wa saa moja unusu usiku wa Jumatano baada ya kuhojiwa kwa saa tatu katika ofisi za EACC mjini Nyeri.

Wapelelezi wa EACC walivamia ofisi na nyumba za Bw Waititu zilizoko jijini Nairobi na Kiambu, ambako walifanya msako uliodumu karibu saa sita.

Baadaye walitoka naye nyumbani kwake Runda na kufululiza hadi makao makuu ya EACC, ambapo alikuwa angali akihojiwa kufikia wakati wetu kuchapisha gazeti jana jioni.

Nyumba yake nyingine iliyo katika mtaa wa Garden Estate pia ilifanyiwa upekuzi na stakabadhi kadhaa zikabebwa.

Kwenye taarifa, Afisa Mkuu wa EACC, Twalik Mbarak alisema Bw Waititu anachunguzwa kwa madai ya kutoa zabuni za thamani ya Sh588 milioni kinyume cha sheria, ufujaji wa fedha za umma na ulanguzi wa pesa.

Kulingana naye, inashukiwa Bw Waititu alitoa zabuni hizo kwa kampuni zinazohusishwa naye mwenyewe na jamaa zake wa karibu.

“Wakati wa upekuzi, ushahidi muhimu ulipatikana unaohusiana na upelelezi unaoendelea,” akasema Bw Mbarak na kuongeza Bw Waititu na washukiwa wenzake walikuwa wanahojiwa zaidi katika makao ya EACC.

Wakati wachunguzi wa EACC walipokuwa wakiendeleza operesheni nyumbani kwa Bw Waititu, Naibu Rais William Ruto alikuwa katika kituo cha redio cha Kameme FM, ambapo aliendelea kumtetea gavana huyo kuhusu madai ya awali yaliyokuwa yametokana na ripoti ya Mhasibu Mkuu, Bw Edward Ouko.

Ripoti hiyo, ambayo ilidai Kaunti ya Kiambu ilitumia mamilioni ya pesa kufadhili shughuli zisizostahili kama vile udumishaji amani Sudan Kusini na shughuli nyinginezo za Ikulu, ilifanya viongozi karibu wote wa Kiambu kujiepusha naye huku baadhi ya wakazi wakiandamana kuonyesha ghadhabu dhidi yake.

Hata hivyo, baadaye Bw Ouko alifafanua kulikuwa na kasoro ambazo ziliathiri pia ripoti za uhasibu za kaunti nyingine kadhaa.

Wapelelezi walifika katika nyumba ya Bw Waititu mtaani Runda dakika chache baada ya saa kumi na moja alfajiri.

Maafisa 10 walipiga kambi katika boma hilo hadi saa sita walipomkamata na wakuwa wamemzuia kwenda kazini.

Mbali na kubeba stakabadhi kutoka nyumbani kwake na afisini, walichukua pia nambari za usajili za magari na stakabadhi nyingine walizopata katika gari la gavana huyo aina ya Toyota Prado.

Wapelelezi pia walivamia ofisi za serikali ya kaunti mjini Ruiru na Thika na wakabeba kabati kubwa ya chuma iliyokuwa imefungwa. Haikujulikana kabati hiyo ilikuwa na nini ndani.