HabariSiasa

Baba Yao atiwa adabu na madiwani

December 19th, 2019 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MADIWANI wa Kaunti ya Kiambu wamepitisha kura ya kumwondoa mamlakani Gavana Ferdinand Waititu Baba Yao kwa matumizi mabaya ya afisi na mienendo mibaya.

Katika aumuzi uliofikiwa Alhamisi katika bunge la kaunti hiyo, jumla ya madiwani 63 kati ya 92 walionga mkono hoja hiyo

Ni diwani mmoja tu alipiga kura ya kupinga hoja hiyo huku wengine 28 hawakuhudhuria kikao hicho.

Madiwani hao walimsuta Bw Waititu kwa kukiuka Katiba, Sheria za serikali ya kaunti, Sheria kuhusu Ununuzi na Uuzaji wa Bidhaa na Huduma za Umma na Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma.

Hoja hiyo iliwasilishwa na diwani wa Ndenderu Solomon na ikaungwa mkono na mwenzake wa Kahawa Wendani Cyrus Omondi.

Akianzisha mjadala kuhusu hoja hiyo Kinuthia aliliambia bunge hilo kwamba Gavana Waititu alifeli kuwajibikia rasilimali za kaunti na kuifanya serikali hiyo kutumbukia katika lindi la madeni ya kima cha Sh4 bilioni.

“Kwa hivyo, vitendo vya gavana viliiweka serikali ya kaunti katika hali mbaya kifedha,” akasema. Bw Kinuthia aliongeza kuwa Gavana Waititu aliajiri wafanyakazi 600 bila kuhusishwa Bodi ya Uajiri wa Wafanyakazi wa Kaunti (CPSB).

Kufuatia hatua hiyo sasa Spika wa Bunge hilo Stephen Ndichu atawasilisha hoja hiyo kwa Spika wa Bunge la Seneti Ken Lusaka ili abuni kamati ya maseneta 10 kuchunguza madai dhidi ya Waititu. Ikiwa seneti itakubaliana na madai kwenye hoja hiyo basi Bw Waituti atakuwa amepigwa kalamu rasmi.