Habari MsetoSiasa

Baba Yao atumia Sh6m kuwatibu wanabodaboda waliopata ajali

June 10th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAHUDUMU wa bodaboda wapatao 55 waliopata ajali watanufaika na ufadhili wa matibabu kutoka kwa Serikali ya Kaunti ya Kiambu.

Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu, alisema tayari serikali yake imetoa Sh6 milioni zitakazogharimia matibabu na vifaa vyote vinavyohitajika katika matibabu ya wanabodaboda hao.

“Baadhi ya wale walioletwa katika hospitali ya Thika Level 5 na ile ya Kiambu Level 5 wamekamilisha zaidi ya miezi miwili na hawana jinsi ya kupata matibabu kwa ukosefu wa fedha,” alisema Bw Waititu.

Aliyasema hayo jana, alipozuru hospitali ya Thika Level 5, alipotoa amri wahudumu hao watibiwe halafu serikali ya Kiambu ilipie gharama hiyo yote.

Dkt David Ndegwa anayewatibu wagonjwa wa mifupa hospitali ya Thika Level 5 alisema hatua hiyo ya kaunti ni ya kusifiwa kwa sababu walioathirika watapokea matibabu ya haraka na chini ya siku nne hivi wataweza kujitembeza wakitumia mikongojo.

“Hospitali imelazimika kununua vifaa muhimu vinavyohitajika ili kufanikisha mpango huo. Sasa tutafanya upasuaji wa dharura na kuona ya kwamba mhusika anapata nafuu haraka iwezekanavyo,” alisema Dkt Ndegwa.

Baadhi ya wahudumu waliopata majeraha mabaya walishukuru hatua ya Bw Waititu, wakisema wanatumaini kurejea makwao hivi karibuni.