HabariSiasa

BABA YAO: Nilikuwa humu humu tu, sikuhepa!

July 29th, 2019 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

BAADA ya mchezo wa paka na panya kushuhudiwa kati ya Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kwa siku mbili, hatimaye gavana huyo alijisalimisha kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Jumapili na kudai hakuwa amekwepa kukamatwa.

Maafisa walikuwa wakimtafuta kwa madai ya ufisadi ambayo yamemhusisha pia mke wake, Bi Susan Ndung’u, lakini wakashindwa kumpata katika nyumba zake zote wanazozijua.

Jaribio lao kumtafuta gavana huyo aliye maarufu kama Baba Yao katika maskani zake za burudani wikendi hazikufua dafu.

Jana, wakili wa gavana huyo, Bw Oliver Kipchumba alisema alikuwa yuko tu humu nchini ila hakuwa mjini ndiposa hangeweza kujisalimisha kwa polisi wakati alipohitajika kufanya hivyo.

“Gavana hakuwa mjini. Alirudi jana usiku ndipo tukaamua kufika kwa EACC asubuhi hii. Haiwezekani mtu yeyote kutoroka mkono wa sheria, hasa akiwa ni gavana…haiwezekani kwamba gavana alikuwa ametoroka,” akasema Bw Kipchumba.

Fununu zilikuwa zimedai Bw Waititu alienda mafichoni ili asilale seli wikendi nzima kabla kufikishwa kortini leo. Kwenye mitandao ya kijamii, wananchi walitania DCI itoe zawadi ya mamilioni ya pesa kwa atakayewaarifu kuhusu mahali Bw Waititu alikuwa.

Majasusi walitumia muda wao mwingi Ijumaa usiku na siku nzima Jumamosi wakimtafuta gavana huyo.

Kabla ajisalimishe mwendo wa saa tatu unusu asubuhi jana, wapelelezi walikuwa wamepiga kambi katika nyumba zake zilizo mitaa ya Runda, Garden Estate na Ridgeways.

Walimtafuta hadi katika mikahawa iliyo mjini Nairobi na vilevile Nakuru, bila mafanikio.

Duru zilisema wapelelezi walikuwa wanafuata mawimbi ya simu zake za mkononi wakafanikiwa kutambua simu moja ilikuwa nyumbani kwake Runda.

Hata hivyo walipowasili katika nyumba hiyo, walipata simu zake zilikuwemo lakini yeye mwenyewe hakupatikana.

Ilishukiwa aliacha simu zake nyumbani kusudi akifahamu fika kwamba kama angezibeba, bila shaka angenyakwa upesi.

Wapelelezi walibainisha pia simu za mkononi za wasaidizi wa gavana huyo na zile za jamaa zake wa karibu zilizimwa wakati huo wote.

Mnamo Ijumaa, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Noordin Haji aliagiza Bw Waititu akamatwe na kushtakiwa kuhusu utoaji zabuni ya Sh588 kwa njia haramu.

Zabuni hiyo ya ujenzi wa barabara ilipeanwa kwa kampuni ya M/s Testimony Enterprises ambayo wakurugenzi wake ni wandani wa Bw Waititu, na tayari walilipwa Sh147.3 milioni Kampuni hiyo ilipewa pia kandarasi zingine za zaidi ya Sh74 milioni.

Bw Kipchumba jana alisema hawakufahamishwa wakati gavana atafikishwa mahakamani.

Mbali na Bw Waititu, mshukiwa mwingine aliyejisalimisha jana ni Afisa Mkuu wa Barabara katika Kaunti ya Kiambu, Bw Luka Mwangi Waihenya.

Washukiwa wengine wanaohusishwa na sakata hiyo walikuwa wamekamatwa awali.

Wanajumuisha Charles Mbuthia ambaye ni mkurugenzi katika kampuni ya Testimony Enterprises Limited na wanachama wa kamati ya kukagua zabuni katika Serikali ya Kaunti ya Kiambu, Joyce Musyoka na Simon Kangethe.

Wengine ambao walikuwa bado wanatafutwa kufikia wakati wa kuchapisha gazeti hili, ni Beth Wangechi, Zacharia Mbugua, Anselin Wanjiku na Samuel Mugo.