Habari Mseto

Babake Farida Karoney azikwa nyumbani Kamobo

October 19th, 2020 1 min read

NA TOM MATOKE

Mazishi ya baba yake Waziri wa Ardhi Farida Karoney, Mzee Edward Karoney yanaendelea katika Kaunti ya Nandi.

Mzee Karoney alifariki kwenye ajali ya barabara iliyotokea mji wa Kapsabet Jumanne.

Alifariki akiwa kwenye hospitali ya Kaunti ya Kapsabet alipopelekwa baada ya kugongwa na pikipiki iliYokuwa imeendeshwa kwa kasi.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Nandi Samson Ole Kine alisema ajali hiyo ilitokea kwenye barabara kuu ya  Kapsabet -Kakamega.

Mkuu huyo wa polisi alisema mwanabodaboda huyo alipelekwa hospitali ya Kapsabet. Mzee Karoney alikuwa ameegesha gari lake karibu na barabara na alipata ajali hiyo alipokuwa akivuka barabara.

Walioshuhudia walisema kwamba mwathiriwa alikuwa akienda kukutana na rafikiye upande mwingine wa barabara alipopata ajali hiyo.

Bw Ole Kine alisema kwamba Mzee Karoney alithibitishwa kufariki alipofika hospitalini.

“Mwathiriwa aliafriki kutokana majeraha na kuvunja damu. Mwendeshaji huyo wa bodaboda bado anapokea matibabu hospitalini,” alisema Bw Ole Kine.

Mwanawe ambaye ni waziri wa ardhi alifikia hospitalini Jumanne asubuhi kabla ya mwili wa babake kufikishwa nyumbani kwao Kamobo.