Habari Mseto

Babake Julie Ward adai kuwa na ushahidi mpya

August 25th, 2020 2 min read

Na STELLA CHERONO

BW John Ward, babake mpigapicha wa wanyamapori Bi Julie Ward aliyeuawa nchini miaka 32 iliyopita anasema ana ushahidi mpya kuhusu mauaji ya mwanawe.

Bi Ward aliuawa mnamo Septemba 1988 alipokuwa ziarani katika Mbuga ya Wanyamapori ya Maasai Mara katika hali tatanishi.

Tangu wakati huo, Bw Ward amekuwa kwenye juhudi za kutafuta ukweli kuhusu mauaji ya mwanawe, ambapo ametumia zaidi ya Sh200 milioni kwenye harakati hizo.

Inakisiwa amesafiri nchini mara 208 tangu alipoanza juhudi za kubaini kiini halisi cha mauaji ya mwanawe.

Bw Ward alikuwa akimlaumu Jonathan Moi, mwanawe marehemu Daniel Moi kwa mauaji hayo. Hata hivyo, Jonathan alishikilia kuwa hakuhusika kamwe kwenye mauaji hayo hadi alipofariki Aprili mwaka uliopita. Alieleza hakumfahamu Julie na hakuwepo kwenye mbuga hiyo wakati alipouawa.

Kwenye mahojiano Jumamosi, Bw Ward alisema baadhi ya mashahidi wametoa ushahidi mpya, hali ambayo huenda hatimaye ikafichua ukweli kuhusu suala hilo.

Bw Ward, ambaye ni raia wa Uingereza, aliliambia gazeti la ‘Mirror’ nchini humo kuwa mashahidi wengi walisema ni baada ya kifo cha Jonathan walipohisi ikiwa salama kwao kutoa ushahidi wao.

Watu watatu walishtakiwa kwa mauaji yake lakini hakuna hata mmoja aliyehukumiwa kufikia sasa.

Awali, wachunguzi kutoka Kenya walisema kwamba Ward, wakati huo akiwa na umri wa miaka 28 aliliwa na simba na baadaye kupigwa na radi.

Wachunguzi hao waliongozwa na Kamishna wa Polisi Philip Kilonzo.

Lakini mwaka mmoja baadaye, babake alitoa ushahidi ulioonyesha mwanawe alibakwa na kuuawa huku mwili wake ukichomwa baadaye.

“Lengo langu tu ni kuhakikisha Julie amepata haki. Tunajua aliyemuua. Tunataka tu kuthibitisha kupitia ushahidi mpya ili kuondoa utata ambao umekuwepo,” akasema.

Alieleza anataka dunia kujua ukweli kuhusu suala hilo kabla yake kufariki.

Ushahidi mpya ambao anadai kuwa nao ni ule unaoonyesha Jonathan alikuwa kwenye mbuga hiyo wakati mwanawe alipouawa.

Akihojiwa kuhusu mauaji hayo, Jonathan alisema hakuwa karibu na mbuga hiyo.

Bw Ward alisema picha za mwili wa mwanawe huwa zinamsumbua akilini mwake hadi sasa, na ndipo huwa anafanya kila juhudi kuhakikisha amepata haki.

“Haikuwa taswira nzuri. Mguu wake ulikuwa umekatwa na kuchomwa, hali iliyoonyesha ilikuwa njama iliyopangwa,” akasema.

Bw Ward pia alisema anafanya mazungumzo na wanafilamu kutengeneza sinema inayoonyesha safari yake kumtafutia haki marehemu mwanawe.