Habari Mseto

Babangu alipenda nyama hasa ya mbavu, Gideon hatimaye afichua

February 11th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Baringo Gideon Moi amefichua Jumanne siri za babake, Rais wa zamani Daniel Moi ambazo yumkini Wakenya hawakufahamu.

Alihutubu katika uwanja wa Nyayo, Nairobi, wakati wa ibada ya kumuaga Mzee Moi, Gideon alifichua vyakula ambavyo Moi alipenda na uraibu wake.

Kinyume cha imani ya wengi kwamba Moi alipenda kula mboga, Seneta huyo wa Baringo alitoboa kwamba babake alipenda kula nyama, hasa ile ya mbavu.

“Huyo Mzee alikuwa anapenda nyama. Siku moja nilimwambia kwamba daktari alimwonya dhidi ya kula nyama, lakini akauliza hivi; ‘unaona daktari hapa?'” akasema seneta Gideon.

Na wakati wake wa mapumziko, hasa baada ya kustaafu, Moi alipenda kutizama vipindi vya Burudani vya Mieleka (WWE).

Mzee alimhusudu mwanamieleka kwa jina Big Daddy aliyefariki mnamo mwaka wa 2005 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.

Moi pia alipenda kutizama mahubiri ya Pasta Billy Graham, raia wa Amerika.

Mhubiri huyu amesifika zaidi kama mmoja wa viongozi wa kidini wenye ushawishi mkubwa zaidi katika karne hii. Alifariki mnamo mwaka wa 2018.

Rais huyo wa zamani ambaye alifariki mnamo Februari 4 atazingwa Jumatano nyumbani kwake Kabarak, kaunti ya Nakuru.