Michezo

Babaye Neymar sasa kulishwa urojo na mwanamitindo Franciely Freduzeski

June 2nd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SANTOS Snr ambaye ni babaye mzazi mchezaji ghali zaidi duniani, Neymar Jr, amejinasia penzi la mwigizaji na mwanamitindo maarufu nchini Brazil, Franciely Freduzeski, 40, ambaye kwa sasa anapanga kumfanya wake wa halali.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, wawili hao wamekuwa wakihusiana kisiri kwa muda mrefu tangu Santos atemane na mkwe Nadine mnamo 2012.

Ingawa Neymar amekuwa akitamani sana kuwaona wazazi wake wakirudiana, Santos mwenye umri wa miaka 55 amesisitiza kuwa amepania kula yamini ya ndoa na Franciely kufikia mwisho wa mwaka huu.

Wawili hao walionekana kwa mara ya kwanza wakiponda raha viungani mwa mji wa Sagrada, Uhispania mnamo Februari 2020.

Kwa mujibu wa Neymar, Santos alimtambulisha kwa Franciely mnamo 2018 baada ya sadfa kuwakutanisha katika mojawapo ya mikahawa ya kifahari jijini Rio, Brazil.

Ni katika hafla hiyo ambapo Santos alimpendekezea Neymar kurudiana pia na kichuna Bruna Marquezine na kukoma kabisa kutoka kimapenzi na mwanamuziki mzawa wa Amerika, Selena Gomez ambaye kwa wakati huo alikuwa akishindana na Soraja Vucelic kuliwania penzi la Neymar, 28.

Santos anafichua mipango ya kumuoa Franciely siku chache baada ya mkewe wa zamani, Nadine, 52, kumtema ‘ben ten’ wake Tiago Ramos, 23, baada ya wiki mbili pekee za kurushana roho.

Nadine alimfurusha Tiago kwenye kasri lake majuzi baada ya kugundua kwamba bingwa huyo wa masuala ya teknolojia ya kompyuta aliwahi kuwa katika mahusiano mengi ya kimapenzi na wanaume wengine kabla ya kuanza kuchovya asali mzingani mwake.

Mbali na kuhusiana kimapenzi na Mauro ambaye ni mpishi mkuu wa Neymar, Tiago aliwahi pia kuwa shoga wa Carlinhos Maia, mwanamume ambaye ni mwigizaji maarufu jijini Rio, Brazil. Neymar aliunga mkono uhusiano huo mpya wa Nadine baada ya mamaye huyo kusisitiza kwamba hakuna yeyote ambaye angeelewa raha aliyokuwa akipata kutoka kwa Tiago.