Habari

Babeli ya Uhuru

July 11th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

BARAZA la Mawaziri la Rais Uhuru Kenyatta limepasuka mirengo minne, hali inayotishia kuzima ndoto yake ya kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo kufikia mwaka 2022.

Migawanyiko hiyo imechochewa na tofauti zilizozuka kati ya Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto tangu handisheki mwaka jana na siasa za urithi wa 2022.

Kulingana na duru ndani ya baraza la mawaziri, mrengo unaomuunga mkono Dkt Ruto ndio wenye idadi kubwa ya mawaziri ukiwa na 11 nao ule wa Rais Kenyatta una saba.

Mawaziri watatu, duru zinaeleza, hawaegemei upande wowote. Hawa wametajwa kuwa Najib Balala, Prof George Magoha na Raphael Tuju.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Peter Munya naye ameelezwa kuwa kwenye kambi yake kivyake. Hii inatokana hasa na kuwa anaonekana kama mgeni kwenye baraza hilo kutokana na kuwa ana chama chake kilichokataa kujiunga na Jubilee.

Duru hizo zilieleza Taifa Leo kuwa katika mrengo wa Rais kuna Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani), Racheal Omamo (Ulinzi), Monica Juma (Masuala ya Kigeni), James Macharia (Uchukuzi), Joe Mucheru (Mawasiliano na Teknolojia), Sicily Kariuki (Afya) na Amina Mohamed (Michezo).

Migawanyiko hii imezua wasiwasi wa uwezekano wa kukwama kwa utekelezaji wa sera za Serikali na hata mikutano ya baraza hilo. Pia mawaziri wanaripotiwa kushikwa na wasiwasi wa uwezekano wa kufutwa kazi iwapo Rais Kenyatta ataamua kulivunja baraza hilo ama kufanya mabadiliko.

Kumekuwepo na miito kwa Rais Kenyatta kuvunja baraza hilo lakini Rais anakabiliwa na kizingiti cha kuwa sharti aafikiane na Dkt Ruto kuhusu mabadiliko kwa kuwa limeundwa chini ya mkataba wa maelewano ya ugavi mamlaka. Rais Kenyatta pia anafahamika kwa kutokuwa makini kuwafuta maafisa wake.

“Kwa sasa baraza hili la mawaziri linakaa kama soko la wachuuzi wa bidhaa tofauti,” waziri mmoja alidokezea Taifa Leo.

Raila alaumiwa

Kinara wa ODM, Raila Odinga analaumiwa na mrengo wa Dkt Ruto kwa mipasuko katika Baraza la Mawaziri, ikihojiwa kuwa ndiye atakayenufaika zaidi kisiasa, iwapo Jubilee itashindwa kutimiza ahadi zake kwa Wakenya ifikapo uchaguzi wa mwaka 2022.

Habari zinaeleza kuwa migawanyiko hiyo inachochewa hasa na siasa za urithi wa 2022, ambapo kila mmoja anataka kujiweka katika nafasi nzuri ya kunufaika na utawala utakaochukua madaraka.

Tayari kumekuwa na madai kutoka kwa Dkt Ruto kuhusu njama ya baadhi ya mawaziri kula njama ya kumuua. Mawaziri waliotajwa ni Bw Munya, Bw Macharia, Bw Mucheru na Bi Kariuki.

Madai hayo yanazua masuala la iwapo Dkt Ruto na mrengo wake wanaweza kuaminiana na kufanya kazi kwa pamoja na wale wanaodaiwa kumpangia kifo.

Duru ndani ya baraza hilo ni kwamba wengi wa mawaziri wameingiwa na wasiwasi mkuu wa jinsi ya kutekeleza majukumu yao ndani ya baraza hili kwa kuwa hawana uhakika wa vile siasa hizi zitaishia.

Kwa sasa, hali ndani ya baraza hilo imeripotiwa kuwa ya taharuki kuhusu hatima yao huku miito ya baraza hilo livunjwe.