Habari Mseto

Babu afariki akimwokoa mjukuu wake

November 12th, 2018 1 min read

Na Benson Amadala

MZEE mwenye umri wa miaka 78 alifariki baada ya kukanyaga waya wa umeme alipokuwa akijaribu kumwokoa mjukuu wake katika Kaunti ya Kakamega.

Kulingana na majirani, mzee huyo aliyetambuliwa kwa jina la Joseph Oyugi Ochieng’, alikanyaga waya huo nyumbani kwake alipokuwa akikimbia kwenda kumwokoa mjukuu wake wa kike aliyekuwa akianika nguo kwenye kamba kijijini Shirere, Jumamosi.Waya huo wa umeme ulikuwa umegusana na kamba ya kuanika nguo.

“Marehemu alitoka nje akiwa amebeba mti aliotaka kutumia kumnasua mjukuu wake kutoka kwa waya wa umeme. Kwa bahati mbaya alikanyaga waya uliokuwa ardhini na akafariki,” Bw Bernard Ogere, ambaye ni jamaa yake alieleza.

Msichana alichomeka na alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kakamega ambapo anapokea matibabu.

Chifu wa lokesheni ya Bukhungu Maurice Muchiti alisema mkasa huo umesababishwa na uzembe wa mafundi wa kuunganisha nyaya waliokuwa wamelipwa kuweka umeme kwenye nyumba mpya iliyojengwa nyumbani hapo.