Makala

Babu mtembezaji watalii ufuoni aapa kushikilia kazi hadi kifo

Na KALUME KAZUNGU August 7th, 2024 3 min read

TWAHA Ahmed Omar ndiye mhudumu wa matembezi ya watalii ufuoni mkongwe zaidi kaunti ya Lamu.

Akiwa na umri wa miaka 80, Bw Ahmed pia ni miongoni mwa wahudumu wakongwe zaidi ambao bado wameshikilia kuendelea kutoa huduma za matembezi ya watalii ufuoni Ukanda wa Pwani ya Kenya.

Licha ya umri wake kusonga hadi kuitwa babu, Bw Ahmed anashikilia kuwa katu hatoiacha kazi hiyo hadi kifo kwani humfanya kujiona yeye bado ni kijana anayefaa kula ujana.

Alianza kujishughulisha na utoaji huduma za watalii ufuoni akiwa umri wa miaka 18 pekee.

Licha ya kisomo chake kuwa cha chini, akiwa aliachia darasa la sita pekee, Bw Ahmed anasema ni kupitia jukumu lake hilo la matembezi ya watalii ufuoni ambapo ameweza kujifunza lugha nyingi za kigeni, ikiwemo Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kitaliano, na pia vijilugha vya mtaani, ikiwemo Sheng.

Kwa sababu yeye tayari ni kutoka jamii ya Waswahili wa asili ya Wabajuni wa Lamu, anaweka wazi kwamba Kiswahili hakikuwa tatizo kwake kukifahamu na kukizungumza kwani anakichukulia kuwa sawa na lugha ya mama.

Mzee Omar, 80, akiwa mwingi wa bashasha wakati wa mahojiano. Picha|Kalume Kazungu

Kwa babu Ahmed, ni kawaida kwake kama ibada kumpata ufuoni akiwa amejifunga kikoi cheusi kiunoni huku akivalia fulana.

Uso wake mara nyingi huwa haukosi tabasamu, hali ambayo mwenyewe anadai huwavutia watalii wengi kusaka huduma zake.

“Nilianza kazi hii karibu miaka 60 iliyopita. Najua wengi wanashangaa kwa nini bado nasukumana kutekeleza majukumu haya yangu licha ya kubugia chumvi nyingi. Hawafahamu naipenda na siiachi kamwe hadi kifo,” akasema Bw Ahmed.

Anashikilia kuwa siri ya kufaulu katika kazi hiyo ni kuinoa tabia yako kwa kuzingatia ukweli na uaminifu na pia ujuzi wa maeneo anayohudumia kwa kuitambua historia ya eneo anakoishi ndani na nje, kujua ni maeneo gani yanafaa kwa matembezi ya wageni, ni wakati gani mwafaka wa wageni au watalii kufurahia maandhari fulani.

Pia anashauri wahudumu kujua kinagaubaga hali ilivyo ya usalama kwa watalii kwenye maeneo unakowatembeza.

“Ukitaka ufaulu kwenye kazi yetu lazima uwe na tabia ya ukarimu. Tabasamu lako ni muhimu kwani ndilo linalovutia na kuwakaribisha watalii. Hutanipata nikiwa na sura iliyokunjamana hata ninapopitia msongo wa mawazo maishani. Kufanya hivyo ni sawa na kuwafukuza wageni,” akasema Bw Ahmed.

Mhudumu huyo mkongwe aidha anachambua na kuchanganua sekta ya utalii ya zamani na ya miaka ya sasa ya karne ya 21 akisema kuna mabadiliko makubwa.

Anasema miaka ya sitini (1960s) na tisini (1990s), sekta ya utalii Kenya ilishuhudia sana ujio wa watalii wa kimataifa.

Bw Ahmed anaeleza kuwa hata wahudumu waliofanya kazi wakati huo hawakuwa wengi ikilinganishwa na miaka ya sasa ambapo kila mmoja, iwe kijana, mtoto na hata mzee utampata akitekeleza majukumu hayo.

“Utapata miaka ya zamani watalii wengi tuliowapokeza hizi huduma za matembezi ufuoni walikuwa ni kutoka ng’ambo. Leo hii utapata sekta ya utalii ikisheheni wageni au watalii wa ndani kwa ndani tu. Utapata watalii kutoka Nairobi, Nakuru, Kisumu, Naivasha na kwingineko wakizuru Lamu kujivinjari,” akasema Bw Twaha.

Mkongwe huyo pia anataja kuimarika kwa teknolojia katika ulimwengu wa leo ambao ni wa utandawazi kuwa jambo linalozidi kuibadilisha sekta ya utalii nchini na duniani kote.

“Kitambo watalii walitegemea sana kuzuru hapa, ambapo walitutumia sana sisi wahudumu wa matembezi ya ufuoni kutafuta hoteli na sehemu zingine za kujivinjari na hayo yote yalimaanisha walitulipa fedha nyingi. Leo hii hilo halipo. Mtalii anaingia tu mtandaoni na kujitafutia hoteli na hata kuikodisha mapema kabla hajafika Kenya,” akasema Bw Ahmed.

Mzee Omar akiashiria anavyotembeza wageni ufuoni Pate bila kuchoka licha ya umri wake mkubwa. Picha|Kalume Kazungu

Pia anataja tabia za kisasa za vijana wengi wanaojiita watembezaji watalii ufuoni kuwa zisizofaa na ambazo zinaharibia sifa wale watembezaji kindakindaki.

Miongoni mwa tabia hizo ni matumizi ya dawa za kulevya na hata kuwa na tabia za ukali au kuwalazimisha watalii kukodisha huduma zao.

Baadhi ya wakazi wanaomfahamu Bw Twaha hata hivyo wanamsifu kuwa mtu roho safi na mpenda wote.

Bw Lali Omar, mkazi wa Kiwayu anasema Bw Twaha ni mjuzi wa karibu maeneo yote ambayo ni vivutio vya watalii si Lamu Mashariki tu bali pia kaunti yote.

“Huyu babu anapendwa na watalii kwa sababu ya ukwasi wake wa taarifa kuvihusu vivutio vya watalii vipatikanavyo Lamu. Utampata kwenye ngome ya Siyu akiwaeleza watalii kuhusu historia yake. Utampata Pate akieleza jinsi himaya ya Sultan wa Uswahilini ilivyovuma karne ya 15 na 16. Utampata Shanga akikueleza kuhusu chimbuko la Wachina pale nakadhalika. Ni mwanahistoria tosha,” akasema Bw Lali.

Adalyn Henry, mtalii kutoka Uingereza ambaye huja Lamu karibu kila mwaka, anasema yeye hupendelea sana kukodisha huduma za babu Ahmed kumtembeza ufuoni na kwenye vivutio vya Lamu kutokana na ukarimu wake.

“Unapokuwa na Bw Ahmed hutaboeka. Atakupa stori za kuvutia kuihusu Lamu hadi uridhike. Hana tabia za usumbufu kwa watalii bali huhakikisha hata kukaa kwetu hapa kunasalia kuwa kwa kumbukumbu,” akasema Bi Henry.

Mbali na Bw Ahmed, mhudumu mwingine mkongwe wa matembezi ya watalii ufuoni Kaunti ya Lamu ni Bw Ziwa Abdalla aliyetinga umri wa miaka 75 kwa sasa.

Bw Abdalla naye ni mzaliwa wa mtaa wa Langoni kwenye mji wa kale wa Lamu.

Amehudumu kama mtembezaji watalii ufuoni kwa miaka 55 sasa.