Habari

Babu Owino aachiliwa baada ya kulipa awamu ya kwanza ya dhamana

January 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameachiliwa huru Jumanne jioni huru kutoka gereza la Nairobi baada ya kutoa Sh2.5 milioni kama awamu ya kwanza ya dhamana aliyopewa ya Sh10 milioni, pesa taslimu.

Mnamo Jumatatu Mahakama ya Milimani iliamuru kwamba Bw Owino alipe Sh10 milioni, pesa taslimu ili aachiliwe huru.

Lakini aliruhusiwa kulipa pesa hizo kwa awamu nne, ambapo sehemu ya pesa hizo zitatumika kulipia bili ya hospitali ya DJ Evolve ambaye jina lake halisi ni Felix Odhiambo.

Owino anatuhumiwa kumpiga risasi DJ katika baa moja mtaani Kilimani, Nairobi.

Mbunge huyo pia aliamuriwa kutotumia pombe na dawa za kulevya katika eneo lolote la burudani katika kipindi chote kesi yake ikiendelea.

Owino alishtakiwa kwa kosa la kujaribu kumuua DJ Evolve mnamo Januari 17 katika kilabu cha burudani kwa jina B-Club.

Kwa mujibu wa Hakimu Mkuu Francis Andayi, Owino alipaswa kulipa dhamana ya Sh10 milioni kwa awamu nne ya Sh2.5 milioni kila moja kwa kipindi cha miezi mitatu.

Familia ya mwathiriwa ilikuwa imepinga kuachiliwa huru kwa Owino, kutokana na sababu za kiusalama.

Mbunge huyo wa chama cha ODM pia alishtakiwa kwa kosa la mienendo mibaya akiwa amejihami.

Hata hivyo, familia ya DJ Evolve ilipinga kuachiliwa huru kwa Babu kwa dhamana.

Mbunge huyo aliwakilishwa na mawakili Danstan Omari na Cliff Ombeta.