Habari za Kitaifa

Babu Owino adokeza kuishtaki serikali kwa kukandamiza haki zake

June 6th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

JUMATANO ilikuwa siku ya furaha kwa Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili Owino almaarufu Babu Owino alipoachiliwa huru na Mahakama Kuu katika kesi iliyomkabili na wafuasi wengine sugu wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya walioshtakiwa kushiriki katika maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha mwaka 2023.

Baada ya Jaji Samwel Mukira Muhochi kuharamisha Kifungu cha Sheria nambari 77(1), Bw Owino na wenzake sita waliachwa na tabasamu katika nyuso zao.

“Leo ukombozi umefika Kenya. Hakuna mwananchi atakayeshtakiwa tena kwa maandamano ya amani,” akasema Bw Owino.

Mawakili Danstan Omari, Ndegwa Njiru na Duncan Okatchi waliambia mahakama kwamba sheria zilizotumika na wakoloni kunyanyasa wapiganiaji uhuru wakiwemo Hayati Mzee Jomo Kenyatta, Paul Ngei, Achieng Oneko, na Kung’u Karumba, imezikwa katika kaburi la sahau.

“Sasa midomo ya Wakenya imefunguliwa na kupewa leseni ya kuandamana na uhuru wa kuongea kufuatia kuharamishwa kwa sheria ambayo maafisa wakuu wa serikali wamekuwa wakitumia kuwakandamiza Wakenya,” akasema Bw Omari.

Bw Okatchi alisema afisi ya DPP ilikuwa imegeuzwa na Serikali kuwa “mkoloni mweusi na kutumika kukandamiza wananchi”.

Bw Owino aliachiliwa huru na hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Lucas Onyina baada ya kufahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka kwamba Kifungu nambari 77(1) cha Sheria ya uchochezi kiliharamishwa na Jaji Samwel Mukira Muhochi wa Mahakama Kuu ya Nakuru.

“Nimeagizwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga nitamatishe kesi hii dhidi ya Bw Owino na wenzake sita kwa vile kipengee cha sheria wanachodaiwa wamekiuka, kiliharamishwa na Jaji Muhochi,” Bw Gachoka alimweleza hakimu Onyina.

Akitoa uamuzi Bw Onyina alisema hawezi kuendelea na kesi dhidi ya mbunge huyu na wenzake kwa vile Mahakama Kuu imetoa uamuzi uliompa mwelekeo.

“Kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu, hii mahakama haiwezi kuendelea na kesi hii. Washtakiwa wote wameachiliwa huru na dhamana walizokuwa wamelipa mahakamani warudishiwe,” Bw Onyina aliagiza.

Bw Owino na mfuasi sugu wa kinara wa Azimio Raila Odinga, Bw Okoth Otieno almaarufu Gaucho pamoja na Tom Odongo Ong’undi, Michael Otieno Omondi, Pascal Ouma, Kevin Wambo na Willis Owino Baraka, walikuwa wameshtakiwa kushiriki katika maandamano yaliyopinga ushuru wa nyumba na ongezeko la bei za chakula.

Saba hao walishtakiwa kuchochea waandamanaji kuharibu mali.

Baada ya kuachiliwa, Bw Owino na wenzake walisema watawasilisha kesi katika Mahakama Kuu kushurutisha serikali iwalipe fidia kwa kukandamiza haki zao na kuteswa na polisi.

Saba hao walikuwa wameshtakiwa kushiriki katika maandamano Juni 18, 2023, na wakati wa SabaSaba mnamo Julai 7, 2023.

Walikuwa nje kwa dhamana.