Bambika

Babu Owino amfagilia Stivo Simple Boy akipendezwa na bongo lake la biashara

January 17th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino amemtunuka sifa msanii na mwanamuziki Stivo Simple Boy akionekana kufurahishwa bongo lake la biashara.

Mara baada ya Bw Owino kuahidi kufanya kazi na msanii huyo ili kumwezesha kupaa hadi viwango vingine, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro naye amependezwa na hatua ya mbunge huyo wa Orange Democratic Movement (ODM).

Bw Nyoro alitania kwamba kwa kutambua juhudi za hasla–Stivo–kiongozi huyo alichotakiwa kuzingatia sasa ni kujiunga na United Democratic Alliance (UDA).

Bw Owino alikuwa amechapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook picha akiwa na msanii Stivo na kusema walifanya mazungumzo ya kina ambayo yaliweka zingatia kwa kuimarisha maisha ya msanii huyo.

Alidokeza mkutano huo kuwa ni maongezi ya kibiashara, wakati ambapo msanii huyo anapania kufungua kiwanda cha Freshi Barida ili kutengeneza sharubati.

“Nilikutana na Stivo Simple Boy. Wazo lake la kibiashara ni kiwanda cha ladha tofauti za sharubati kwa jina Freshi Barida. Tukuze Simple Boy,” akaandika Bw Owino.

Naye mbunge mwenzake, Bw Nyoro wa upande wa serikali alichangia kwenye chapisho hilo akimpa hongera.

“Vizuri sana kaka. Endelea kukuza ubunifu na bidii ya mahasla. Naona ni kama uko karibu kuingia chama tawala,” alichangia Bw Nyoro wa UDA ambacho ndicho kikubwa katika muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Mashabiki wengine kwenye ukurasa huo walimpongeza Bw Owino na kuahidi kumshika msanii huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikiri kutofaidika pakubwa kutokana na kazi zake za muziki licha ya kazi hizo kushabikiwa na wengi.

“Babu utakuwa mtu wa maana katika nchi hii. Siwezi kusubiri kukuita Mtukufu Rais,” akachangia Tony Mwangi.

Naye Lisa Hany alitaka kufahamu ni wakati gani ataonja sharubati hiyo.

“Popote nitapata bidhaa hiyo, itabidi ninunue na kumtangaza huyu jamaa. Ana maono,” akachangia Lisa Hany

Mnamo Aprili 2022, Stivo alizuka na neo Freshi Barida akidai yeye kajaliwa ubunifu wa kupanga na kuita maneno yakakubalika.

Ni kutokana na kauli hiyo ambapo baadaye aliachia ngoma kali.