Habari

BABU OWINO: Hata Uhuru na Ruto wakija kuwania Embakasi nitawabwaga asubuhi

March 2nd, 2018 1 min read

Na MWANDISHI WETU

DAKIKA chache baada ya mahakama kuu ya Milimani, Nairobi kufutilia mbali ushindi wa mbunge wa Embakasi Mashariki Bw Paul Ongili alamaarufu Babu Owino, mwanasiasa huyo amesema kuwa ana wafuasi wengi sana na hata Rais Uhuru Kenyatta au Naibu wake anaweza kuwabwaga wakija kuwania ubunge katika eneobunge lake.

Babu Owino ndiye mwanasiasa wa tisa kuangukiwa na shoka la kupokonywa ushindi na mahakama, baada ya mlalamishi Francis Mureithi kuwasilisha kesi kupinga ushindi wake.

Mahakama Kuu iliamuru kuwa uchaguzi wa Agosti 8, 2017 ulikumbwa na kasoro nyingi na ukiukaji wa sheria za uchaguzi.

Bw Mureithi alilalama kuwa kulikuwa na matokeo tofauti katika fomu za kunakili idadi ya kura.

Kupitia kwa wakili wake Ham Lagat, Bw Mureithi aliambia mahakama kuwa fomu hakikuweza kuthibitishwa, jambo lililofanya matokeo katika Fomu 35A kukosa kuwiana na yale yaliyoko katika Fomu 35B.

Babu Owino akiwa katika Mahakama Kuu ya Milimani afuatilia kesi iliyomkabili Machi 2, 2018. Ushindi wake ulifutwa na akaagizwa alipe gharama ya Sh5 milioni. Hata hivyo, ameapa kukata rufaa. Picha/ Richard Munguti.

Jaji Joseph Segon alikubaliana na wakili huyo na kuamuru ilikuwa viguma kutambua mshindi.

Akihutubia wanahabari nje ya mahakama Ijumaa, Babu Owino alisema ushindi wake ulifutwa kwa kuwa amekuwa akipinga utawala wa Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto.

“Kila Mkenya anaelewa kuwa kufutwa kwa ushindi wangu ni ishara ya wazi ya vita ninavyopigwa na Rais na Naibu Rais kwa kupinga mbinu zao za utawala.

Hata Uhuru na Ruto wakija kuwania ubunge Embakasi Mashariki, nitawabwaga asubuhi. Kile ambacho hakiwezi kumuua mja ndicho kinachompa nguvu zaidi,” akasema mwanasiasa huyo wa chama cha ODM.