Makala

Babu Owino: Ruto anavalia saa ya Sh10 milioni, aiuze alipe madaktari

April 10th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Embakasi Mashariki, Paul Ongili Owino, almaarufu Babu Owino, anadai kwamba Rais William Ruto anamiliki saa yenye thamani ya Sh10 milioni na anapaswa kuiuza ili kusaidia kuangazia kilio cha madaktari waliogoma.

Mwanasiasa huyo mzushi anasema Rais Ruto hapaswi kusema serikali yake haina pesa, wakati ambapo anavalia pambo la bei ghali.

Kwenye video, mbunge huyo ambaye ni mwanachama wa chama pinzani cha ODM, anaskika akisema Dkt Ruto anapaswa kuuza saa hiyo na atumie mapato yake kulipa madaktari.

“Niliskia Ruto akisema hana pesa kulipa madaktari. Waendelee na mgomo. Huwezi ukatueleza kama Rais eti huna pesa kulipa madaktari ilhali saa unayovalia ni yenye thamani ya Sh10 milioni. Iuze ulipe madaktari,” Babu Owino akasema.

Wiki hii, ni juma la tatu madaktari wakiendeleza mgomo wao wa kitaifa, ambapo wanashinikiza matakwa ya mktaba wa makubaliano yao – CBA 2017, kati yao na serikali, yatimizwe.

Baadhi ya matakwa hayo ni nyongeza ya mshahara na madaktari waliofuzu japo wangali kwenye mafunzo waajiriwe na serikali, kati ya mengine.

Rais Ruto, hata hivyo, mnamo Jumapili, Aprili 7, 2024 alivunja kimya chake kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea akisema serikali yake haitaafikia matakwa yao kwani haina pesa.

Hata hivyo, kiongozi wa nchi aliahidi kuwa zaidi ya madaktari 1, 500 wanafunzi waliofuzu na kuendelea kunoa makali katika hospitali mbalimbali wataajiriwa.

Babu Owino amemkosoa akidai hapaswi kutumia Biblia kupuuzilia mbali kilio cha madaktari.

“Ulisema, ukinukuu Biblia, baba anapaswa kuachia wanawe urithi kwa kuwekeza. Biblia hiyohiyo, Kitabu cha Mathayo 7:9-12, imesema, ‘Ikiwa mtoto amekuomba mkate usimpe jiwe, na anapokuomba samaki utampa nyoka kweli?’ Hivyo basi, wanao ambao ni madaktari wamekuomba samaki na mkate, wape. Wape pesa,” mbunge huyo akaambia Rais.

Babu Owino ambaye ni mwandani wa kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, alihoji kuwa kinyume na tamko la Rais, Kenya ina pesa za kutosha.

“Kenya ina pesa; uliongeza ushuru. Isitoshe, ulisafiri ng’ambo kukopa. Pesa ziko Kenya. Lipa madaktari ili watu wetu wasife. Ukizuru hospitali, watu wanafariki kwa sababu ya kukosa dawa, madaktari na huduma,” alifafanua.

Dkt Ruto ameweka wazi mara kadhaa kwamba kamwe hatachukua mikopo kulipa wafanyakazi.

Madaktari kupitia Katibu Mkuu wa Muungano wao, KMPDU, Dkt Davji Attellah, wameapa kutorejea kazini hadi pale matakwa yao yatakapoafikiwa.

Jitihada za Wizara ya Afya kuzungumza na KMPDU zimeashiria kuambulia patupu.