Habari Mseto

Badi kuendelea kuhudhuria vikao vya mawaziri

November 18th, 2020 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

MKURUGENZI wa Shirika la Huduma za Jiji la Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohamed Badi ataendelea kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri, baada ya Mahakama Kuu kukosa kutoa amri ya kusimamisha kwa muda hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kumjumuisha kwenye vikao hivyo.

Bw Badi alijumuishwa kwenye baraza la mawaziri mnamo Septemba 10, 2020 baada ya kula kiapo cha siri kwenye hafla iliyoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinywa na kuhudhuriwa na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Hata hivyo, mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome alielekea mahakamani kupinga hatua hiyo, akisema Rais Kenyatta hakushirikisha bunge kwenye uteuzi huo kwa kuwa Bw Badi alipaswa kuhojiwa na asasi hiyo jinsi mawaziri hufanyiwa kabla ya kuteuliwa rasmi.

Kesi hiyo ilipotajwa jana, Jaji Anthony Mrima alielezwa kuwa mbunge huyo hakuwa amewasilisha hoja zake kwa maandishi jinsi alivyoamrishwa mnamo Oktoba 6, 2020. Pia wakili wake, Bw Stephen Gitonga hakuwa amewasilisha stakabadhi za malalamishi yake kwa Mwanasheria Mkuu na Bw Badi kwa muda wa siku tatu jinsi korti ilivyoamrisha.

Jaji Mrima aliamrisha kesi hiyo isikizwe Desemba 2 wakati pande zote zitawasilisha utetezi wao.

Bi Wahome alielekea kortini mnamo Septemba baada ya Ikulu kutoa taarifa za kuarifu umma kuwa Bw Badi ataanza kuhudhuria mikutano ya baraza la mawaziri.

Kesi hiyo ilitajwa kama ya dharura na iliyofaa kusikizwa na kuamuliwa haraka kwa kuwa suala la utata lilihusisha afisi ya Rais. Bi Wahome alishikilia kuwa hatua ya kumjumuisha Bw Badi kwenye vikao hivyo ilikuwa haramu na inayokiuka katiba, ndipo akataka korti iibatilishe.

Mbunge huyo wa Jubilee anayeegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ pia alishutumu Rais kwa kutohusisha bunge kumpiga msasa Bw Badi, akisema hiyo inakiuka sheria kwenye katiba.

“Rais atateua mawaziri baada ya kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa,” kinasema kifungu cha 152, ibara ya pili.”

Bi Wahome anasema uamuzi wa Rais unaashiria kuwa utendakazi wa Bw Badi haufai kupigwa msasa na wabunge kwa kuwa hawakuidhinisha uteuzi wake kwenye baraza la mawaziri.

Kando na hayo katiba inatoa mamlaka kwa Bunge la Kitaifa kuangazia utendakazi wa Rais, Naibu Rais, maafisa wa serikali na kuanzisha mchakato wa kuwaondoa afisini iwapo hawatekelezi majukumu yao ipasavyo. Kwa kifupi jukumu kubwa la bunge ni utunzi wa sheria na upigaji msasa utendakazi wa maafisa wanaosimamia idara mbalimbali za serikali.

Aidha mbunge huyo anayehudumu kipindi chake cha pili anasema kwa kumjumuisha jenerali wa jeshi kwenye baraza la mawaziri, Rais alikiuka sheria kwa kuruhusu mgeni asiyetambuliwa kikatiba kushiriki mikutano ya siri ya kuamua masuala muhimu ya kitaifa.

“Hatua ya Rais ni kinyume cha katiba na inafaa kuzimwa. Kwa sasa baraza la mawaziri linajumuisha mtu ambaye hajafuata kanuni zinazohitajika kikatiba. Kwa hivyo baraza la mawaziri la sasa ni haramu,” akasema kwenye stakabadhi zilizowasilishwa kortini.

“Meja Jenerali Badi amejumuishwa kwenye baraza la mawaziri bila sheria kufuatwa jinsi ilivyo kwenye katiba. Serikali ya sasa imebuniwa bila mchakato unaohitajika wa kisheria kufuatwa,” akasisitiza.

Mwanasiasa huyo anashikilia kuwa ujumuishaji wa Bw Badi kwenye baraza la mawaziri hauna msingi wowote kisheria.