Siasa

Bado ana risasi?

January 11th, 2024 3 min read

NA MOSES NYAMORI

KINARA wa Upinzani Raila Odinga ameanza mikakati ya kujijenga upya kisiasa huku dalili za mapema zikionyesha huenda akabuni muungano mpya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Bw Opiyo Wandayi amefichua kuwa huenda wakautema muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na kuanza ushirikiano mpya wa kisiasa au hata kuupanua muungano wenyewe.

Bw Odinga alitumia muungano wa Azimio kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 ambao Rais William Ruto aliibuka mshindi.

Vinara wengine wa Azimio ni Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (Narc Kenya) na Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Wandayi alieleza bayana kuwa iwapo Bw Odinga ataamua kuwania urais kwa mara ya sita, chama cha ODM kitamuidhinisha na kumuunga mkono ili atimize azma yake.

“Hakuna mipaka katika idadi ya kuwania urais. Unaweza kuwania urais hata mara 100 na pia ni lazima niweke wazi kuwa Raila hajawahi kupoteza uchaguzi wowote,” akasema Bw Wandayi.

“Kwa hivyo, suala kuhusu idadi ambayo Raila amewania urais halina msingi. Unajua akiamua kusimama, kama mfuasi wake na mwanafunzi wake wa kisiasa, lazima nitamuunga mkono,” akaongeza.

Aidha, Bw Wandayi ambaye pia ni mbunge wa Ugunja, Siaya, alisema kuwa hakuna uhakika iwapo Azimio itadumu hadi 2027 kwa kuwa kuna uwezekano viongozi wengine watajiunga na kambi ya upinzani na kuipa sura mpya.

“Azimio inaweza kuwa vuguvugu kubwa zaidi na hilo linaweza kusababisha hata jina libadilishwe. Liwe ni vuguvugu gani, baada ya wao kuamua mwaniaji wao wa urais, sisi sote tutamuunga mkono atakayepokezwa,” akasema Bw Wandayi.

Iwapo Bw Odinga ataamua kujitosa debeni katika uchaguzi wa 2027, atafanya hivyo akiwa na umri wa miaka 82.

NEB

Mnamo Jumatano, Bw Odinga mwenyewe alionekana kuanza kujiandaa kwa kinyang’anyiro cha 2027 baada ya kutimua Bodi ya Uchaguzi ya ODM (NEB). Bodi hiyo ilikuwa ikiongozwa na Seneta Maalum Catherine Mumma.

Soma Pia: Raila apangua mfumo wa usimamizi ODM kuzima blanda za uteuzi

Uamuzi wa kutimua bodi hiyo ulifanyika wakati wa mkutano wa kamati simamizi ya ODM iliyoongozwa na Bw Odinga.

Wengine ambao walitimuliwa ni Abdulahi Diriye na Syntei Nchoe.

Emily Awita na Richard Tairo nao walisazwa huku duru zikiarifu kuwa Bi Awita anapigiwa upato kutwaa wadhifa wa mwenyekiti wa bodi ya kura ya chama hicho.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema kuvunjwa kwa bodi hiyo na mapendekezo ya wanaostahili kushikilia nyadhifa zilizosalia wazi kuidhinishwa, kunalenga kuhakikisha kuwa ODM inalinda ugatuzi.

“Haya mapendekezo yatawasilishwa kwa ngazi za chama ili yaidhinishwe rasmi ndipo yawiane na katiba ya chama,” akasema Bw Sifuna.

Mabadiliko hayo yanaonekana kama mbinu ya kuipiga jeki ODM na uwaniaji wa Raila katika uchaguzi wa 2027.

Mnamo Julai 2023, Bw Odinga aliongoza mkutano uliojaa hisia kali wa kutathmini jinsi chama kilivyoendeshwa katika uchaguzi wa 2022.

Ni wakati wa mkutano huo ambapo bodi ya Bi Mumma ilikashifiwa kwa kuingiza doa kwenye mchujo wa ODM na pia kutolinda kura za Bw Odinga wakati wa uchaguzi mkuu.

Hii si mara ya kwanza bodi ya ODM kutimuliwa; hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Raila kulemewa katika kura za 2017.

Kauli ya Bw Wandayi huenda ikaibua mtafaruku ambao umeanza kushuhudiwa katika kambi ya Azimio baada ya baadhi ya wafuasi wa Raila kuanza kumpigia debe awanie tena 2027.

Mnamo Jumanne, Raila alikutana na mwanasiasa na mfanyabiashara Jimi Wanjigi ambaye walitengana naye uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

Bw Wanjigi amekuwa kati ya wanasiasa ambao wamekuwa wakitishia kuongoza maandamano nchini kupinga sera za serikali anazodai zinawaumiza raia kiuchumi.

Raila alipokuwa akisherehekea kutimiza umri wa miaka 79 katika eneo la Malindi, Kaunti ya Kilifi mnamo Janauri 7, mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe alisema, “Baba bado ni chaguo la Azimio katika uchaguzi mkuu unaokuja.”

Bw Murathe alionekana kumlenga Bw Musyoka ambaye ameazimia kuwa kamwe hawezi tena kumuunga mkono Raila kwa mara ya nne baada ya kufanya hivyo, katika uchaguzi wa 2013, 2017 na 2022.

“Mawanda ya kisiasa huenda yakabadilika na wanasiasa kujiunga na kambi mbalimbali kati ya sasa hadi uchaguzi mkuu ujao. Pia 2027 ni mbali ila tutamuunga mkono atakayepeperusha bendera ya Azimio au muungano wowote tutakaokuwa ndani,” akasema Bw Wandayi akirejelea vitisho vya Bw Musyoka vya “kutosimama” na Raila tena.

Aidha, mbunge huyo alisema kuwa kufikia Machi 2024, uongozi wa ODM, chama anachoongoza Bw Odinga, utatathmini mahali ambapo mchakato wake wa kuwasijili wanachama wapya utakuwa umefika kabla ya kutangaza tarehe ya uchaguzi wake wa mashinani.