Habari Mseto

BADO MAPAMBANO! Karua asema ataelekea JSC

August 7th, 2019 2 min read

[email protected]

Na MARY WANGARI

VITA vya kung’ang’ania kiti cha ugavana cha Kirinyaga kati ya Gavana Anne Mumbi na Martha Karua havielekei kuisha hivi karibuni huku mwanasheria huyo akielekea Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) baada ya kutofautiana na uamuzi wa Mahakama ya Juu uliotolewa Jumanne.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha runinga Jumanne usiku, kiongozi huyo wa Narc-Kenya aliofautiana na uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu zaidi uliotibua juhudi zake za kumng’atua mamlakani Gavana wa Kirinyaga, akisema alinyimwa haki na “nimetamaushwa.”

“Huwa unaenda kortini ukiwa tayari kukubali uamuzi baada ya kumaliza mfumo wote wa haki. Kukubali hakumaanishi kuamini hukumu iliyotolewa. Mfumo wetu wa sheria unasema kwamba hii ndiyo korti ya juu zaidi lakini si lazima niiamini. Ni mwisho wa safari kwa kubatilisha uchaguzi lakini si mwisho wa safari kwa kuwasilisha malalamishi. Kuna mbinu nyingine kadha,” akasema Karua.

“JSC ni mojawapo ni mojawapo ya njia hizo. Ninaelekea huko na sitafafanua kuhusu suala hili. Jaji anayehusika anajua kuhusu haya kwa sababu kuna mambo yaliyotendeka ambayo hayakupaswa kutendeka,” alisema Bi Karua akifichua kwamba kuna mashirika ya mabwanyenye katika mfumo wa mahakama yanayoshirikiana na watu fulani kuiba ushahidi.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kugombea urais pia ameahidi kukabili mfumo wa mahakama nchini na kupiga vita mashirika hayo ya mabwanyenye pamoja na udhaifu uliopo katika mfumo wa mahakama nchini.

Aidha, alidai kwamba Mahakama ya Juu ilitatizika kutafuta suala la kiutekelezaji katika kesi yake na ikajiepusha na kuangazia masuala nyeti katika juhudi zilizodhamiria kumnyima haki.

“Sidhani uamuzi huo uliangazia masuala husika. Mahakama ya Juu iling’ang’ana kutafuta vijisababu vya kiutekelezaji ili isishughulikie masuala. Ikiwa wangeshughulikia masuala, hakuna jinsi wangepata uamuzi mwingine ila kututimizia ombi tulilowasilisha,” alisema.

Hisia za mwanasheria huyo zilijiri saa chache baada ya uamuzi uliotolewa na Jaji Isaac Lenaola wa kutupilia mbali kesi yake dhidi ya Gavana wa Kirinyaga kwa msingi wa kukosa ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yake kwamba, Uchaguzi Mkuu 2017 ulisheheni visa vya ulaji rushwa katika vituo zaidi ya 100 katika Kaunti ya Kirinyaga.

Punde baada ya uamuzi huo, Karua alijitosa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo alielezea masikitiko yake akisema kwamba vita vyake vya kutetea haki vitaendelea.

Akimjibu mmoja wa wafuasi wake kwenye Twitter, Karua alifichua kwamba kamwe hatamuunga mkono gavana Waiguru kwa sababu itakuwa sawia na kuunga mkono ukosefu wa haki.

Kwa upande wake gavana Waiguru alimtaka Kiongozi wa Narc Kenya kusonga mbele huku akisubiri uchaguzi wa 2022 akisema kwamba sasa angeweza kumakinika katika kuwahudumia wakazi wa Kirinyaga.

Uamuzi wa Jumanne ulijiri takriban miezi minane, baada ya Karua kuiendea Mahakama ya Juu kufuatia pigo kuu alilopata kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, ambapo jopo la majaji watatu, lilitupilia mbali malalamishi yake kwamba, alinyimwa muda wa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba kulikuwepo na visa vya ukiukaji sheria katika uchaguzi wa ugavana Kirinyaga mnamo 2017.