Michezo

Badoer asema Wazito itawasajili wachezaji chipukizi

July 15th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

MMILIKI wa Wazito Ricardo Badoer ametangaza kwamba timu hiyo sasa itawasajili wanasoka chipukizi wakati huu wa dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji.

Badoer amesema klabu hiyo haitawaendea wachezaji tajika wenye majina jinsi ilivyofanya wakati wa dirisha la uhamisho lililopita, akielezea matumaini yake ya makinda kusaidia Wazito kuwinda ubingwa wa KPL kwa mara ya kwanza msimu ujao.

“Mpango wetu utakuwa tofauti mara hii. Tunatazamia kuwasajili wachezaji wachanga ambao wana msukumo wa kutambisha Wazito kwenye mashindano mbalimbali. Tunataka tu wachezaji wenye ari na lengo la kutusakatia kabumbu,” akasema Badoer kupitia mtandao wa klabu.

Akaongeza: “Hatutawasajili wachezaji tajika mara hii. Lengo letu ni kuwapata wachezaji wachanga ambao wana kasi na hawatatugharimu hela nyingi ilhali hawaleti matokeo mazuri.”

Haya yanajiri baada ya timu hiyo kuwatimua wachezaji si chini ya 12 wiki jana kwa kutowajibika vyema uwanjani na pia athari za virusi vya corona kwenye biashara za bwanyenye huyo.

Baadhi ya wachezaji ambao walifukuzwa Wazito ni wale ambao walikuwa waking’aa kwenye timu zao na walisajili tu wakati wa dirisha fupi la uhamisho mnamo Januari.

Wachezaji kutoka hapa nchini waliooneshwa mlango ni Victor Ndinya, Teddy Osok, Derrick Otanga, Lloyd Wahome, makipa Steve Njung’e na Kevin Omondi.

Wale wa kigeni Augustine Otu, Piscas Kirenge, Issioffu Bourahana na Paul Acquah.

Mshambulizi matata Paul Kiongera naye aliondoka baada ya uongozi wa Wazito kugoma kuendelea na mazungumzo ya kumwongezea kandarasi yake iliyotamatika mnamo Juni.

Kocha Stewart Hall pia aliondoka klabuni kupitia makubaliano na Badoer. Hall alikwamua Wazito vilivyo na hata kuwasaidia kuondoka kwenye eneo hatari la kushushwa ngazi.

Wazito wanashikilia nafasi ya 13 kwenye msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 20 baada ya raundi 23. Ligi bado imesimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na janga la virusi vya corona lililotua nchini kwa mara ya kwanza Mnamo Machi 13.