Habari Mseto

Baharia afariki, wawili waokolewa baada ya mashua kuzama baharini Lamu

January 17th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

BAHARIA mmoja amefariki huku wengine wawili wakiokolewa pale mashua yao walimokuwa wakisafiria ilizama katika Bahari Hindi eneo la Matondini, Kaunti ya Lamu.

Mabaharia hao watatu walikuwa kwenye harakati za kuvuka kutoka kisiwa cha Matondoni kuelekea kisiwa kidogo cha Kisisi kabla ya mashua yao ndogo kukabiliwa na mawimbi makali na dhoruba baharini na kupinduka.

Akithibitisha ajali hiyo, Afisa Msimamizi wa Idara ya Kukabiliana na Majanga, Kaunti ya Lamu, Bw Kupi Shee, amesema mabaharia wawili walionusurika kifo walifaulu kuogelea hadi nchi kavu punde ajali hiyo ilipotokea.

Mwendazake ambaye alitambuliwa kwa jina, Santa Masha, 25 anadaiwa kushindwa kuogelea, hivyo kufa maji baharini.

Bw Shee alisema mwili wa mwendazake umepatikana kupitia juhudi za wapigambizi wa kikosi cha idara ya majanga cha kaunti ya kwa ushirikiano na wale wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini (KRCS).

Alisema mwili wa mwendazake ulipelekwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ya King Fahad mjini Lamu ilhali walionusurika pia wakikkimbnizwa kwenye hospitali hiyo kupata huduma ya kwanza.

“Ni kweli mmoja wa mabaharia kwa jina, Santa Masha amekufa maji baada ya mashua yao kuzama baharini eneo la Matondoni huku wengine wawili, Mateso Karisa na Amani Mganda wakifaulu kuogelea hadi nchi kavu na kuokoa maisha yao. Mashua hiyo ilishindwa kustahimili mawimbi makali na dhoruba baharini hivyo kupinduka. Tayari mwili wa mwendazake umepatikana baharini na kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya King Fahad,” amesema Bw Shee.

Ajali hiyo pia imethibitishwa na Afisa Mshirikishi wa Msalaba Mwekundu, tawi la Lamu, Bi Kauthar Alwy aliyesisitiza haja ya mabaharia na wavuvi baharini kuwa makini wanapotekeleza shughuli zao msimu huu ambapo kunashuhudiwa mawimbi makali kwenye Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu.

“Shughuli za kuutafuta mwili wa baharia aliyepotea baada ya mashua yao kuzama zimesitishwa hasa baada ya mwili wa baharia huyo kupatikana. Wenzake wawili walioogelea hadi nchi kavu wako shwari na wanaendelea kupokea huduma ya kwanza kwenye hospitali ya King Fahad. Cha msingi ni mabaharia na wavuvi wawe makini baharini msimu huu ambapo kunashuhudiwa mawimbi makali na upepo,” amesema Bi Alwy.