Bambika

Bahati aibuka na shoo mpya ya ‘The Bahati Empire’

June 7th, 2024 1 min read

NA MARGARET MAINA

MWANAMUZIKI aliyejiongeza maarifa kuwa nyota wa vipindi vya uhalisia, Kevin Bahati, ametangaza uzinduzi rasmi wa kipindi cha Reality TV kinachoitwa ‘The Bahati Empire’.

Kipindi hiki kipya kinachoweka zingatio kwa Bahati na familia yake, kinaanza rasmi Ijumaa kwenye Netflix.

Bahati, ambaye pia ndiye mwanzilishi wa lebo ya muziki ya EMB, alishiriki trailer ya kipindi cha Reality TV ambacho kinajumuisha The Murayas, Karen Nyamu, Jalang’o, na Pasta Lucy Natasha miongoni mwa wengine.

Tangazo hilo lilitokea baada ya saa 24 za kujaribu kujizolea umaarufu zaidi kwa kutuma ujumbe wa kipekee ambao uliacha mashabiki wakijaribu kufikiria kilichokuwa kikiendelea kwa maisha ya mwanamuziki huyo.

Katika ujumbe wake, Bahati alijisifu akidai kuwa familia yake ndio ya kwanza nchini Kenya kuwa na kipindi cha Reality kwenye Netflix.

“Tulikuwa familia ya kwanza nchini kuwa na reality kwenye kituo cha runinga cha nyumbani (Being Bahati kwenye NTV) na sasa tunaweka historia kama familia ya kwanza ya Kenya kuwa na kipindi cha Reality kwenye Netflix. Mungu Atukuzwe,” akasema Bahati.

Aliongeza kwenye Instagram, “Najua nyote mlitukosa kwenye TV.”

Bahati na mkewe Diana Marua wanafahamika kwa kufahamisha umma kinachojiri maishani mwao ama kiwe ni cha furaha au cha kutafakari kuhusu maisha.