DOMO: Bahati asiye na bahati!

DOMO: Bahati asiye na bahati!

NA MWANAMIPASHO

ILA huyu dogo Kevin Bahati hutuona tukiwa malenge sana sio?

Wakati mwingine huwa nashindwa jamaa anavyowaza. Sishangai nikiona kinachomkuta. Simhurumii kwa kinachomkuta. Isitoshe, sina kinyongo na msela.

Bahati nimefanikiwa kutangamana naye mara sio moja na nitasema kitu kimoja kumhusu jamaa, ana tabia za njama na hila ama uhuni.

Hayo yanayomkuta itakuwa ni ‘karma’ inamweka sawa. Tena kwa mtu kama huyu aliyeanza usanii wake kwa unyenyekevu akiimba nyimbo za kumtukuza Mungu, alihitaji subra sana kutopoteza rada.

Lakini baada ya kupata umaarufu na ustaa, akapagawa, akaiona dunia ni yake, akajihisi na yeye ni mungu.

Leo ‘karma’ imemlazimu kunyenyekea.

Nimewasikia watu kadhaa wakimlalamikia Bahati.

Nitaanza na mimi. Miaka michache iliyopita alipokuwa akijaribu kumsukuma msanii wa injili Denno, jamaa alinipigia simu akitaka niende kumfanyia mahojiano. Nilichomwomba ni usafiri wa kufika nyumbani kwake. Jamaa akanigeuzia kiswahili na kuanza kuniuliza bosi wangu ni nani huku akitishia kuwapigia simu wanishurutishe nifanye anavyotaka yeye. Kwa ujeuri nilimjibu ‘We jibambe’.

Bahati hata naye ukimtaka akupe wasaa wa mahojiano, huwa ni sawa na kupanda mchongoma. Atakuzungusha, wueeh! Ana dharau na kiburi cha ustaa jamaa.

Lakini nikiachana na hamsini zangu naye, utakuwa umeshasikia Eddie Butita akimcharukia jamaa jinsi alivyomwibia wazo na kulifanya lake. Butita alikuja na wazo la shoo ya kupika, akawasaka wadhamini na kumtaka Bahati na mkewe kuwa kama host wa shoo ile. Baada ya miezi michache Bahati akakimbia na wazo na kulifanya lake.

Ninajua aliwahi kufanya hivyo tena kwenye shoo ya Being Bahati iliyokuwa ikipeperushwa na NTV.

Baada ya msimu mmoja wa Reality Show hiyo kupeperushwa, Bahati na produsa Eugene Mbugua wakatibuana baada ya jamaa kukiuka mkataba na kwenda kuanzisha shoo yake The Bahati Reality Show. Ilionyeshwa season moja kabla kufutiliwa mbali. Haijawahi kula shavu tena kwingine au kokote kule. Hizi ndizo hulka za huyu jamaa.

Leo nikimsikia analilia tiketi ya chama cha Jubilee kugombea ubunge wa Mathare, nacheka sana. Miezi miwili baada ya kulia alipoombwa apishe wakubwa wake, jamaa aliita wanahabari na kujitetea kweli kweli. Machozi yalimtiririka ungedhani alikuwa anaumwa na macho. Wana Azimio wakamsikiliza na kumrejeshea tiketi. Juzi kapokonywa tena angalau raundi hii alijitahidi kuyazuia machozi yake. Sasa tena nimemsikia akidai walimpa ofa ya Sh50 milioni ili ampishe mgombea mwingine lakini amekataa. Hajapewa kiti na tayari amezidisha dozi yake ya unafiki. Huyu akipewa fursa ya kuwa mbunge, anaweza akafanya lolote bila ya kujali.

Lakini pia jamaa atakuwa ni zuzu. Nani atakupa kiasi kama hicho cha hela ukatae? Isitoshe, huo ni mshahara wa mbunge kwa miaka mitano. Kama kweli wamempa hela hizo ni kwa nini basi aendelee kuwa king’ang’anizi? Na kama Bahati anajiamini anapendwa na wananchi wa Mathare, ni kwa nini basi asiwe mgombea huru? Huyu ni Bahati asiye na bahati. Willy Paul kamshauri arudi waimbe. Nafikiri huo ni ushauri mzuri.

  • Tags

You can share this post!

Nitafurusha jeshi la Uganda kutoka Migingo – Raila

Mwanamume ashtakiwa kudai kwa fujo

T L