Michezo

BAHATI YA VAR: Manchester United wapigana kufa kupona hadi wakafuzu robo fainali

March 8th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

MANCHESTER United na Porto walibahatika kuingia robo-fainali ya taji la Klabu Bingwa Ulaya, ingawa kupitia teknolojia ya VAR dhidi ya Paris Saint-Germain na AS Roma mtawalia, Jumatano.

Nyota wa Brazil Neymar alikashifu VAR na kutaja uamuzi wake wa kuipa United penalti iliyofungwa na Marcus Rashford na kubandua nje PSG kama “aibu kubwa.”

Rashford alipachika penalti hiyo iliyoingiza United katika robo-fainali kupitia bao la ugenini dakika ya mwisho baada ya kushinda mechi ya marudiano 3-1 jijini Paris, Ufaransa. PSG ilitawala mechi ya mkondo wa kwanza 2-0 nchini Uingereza.

Fred (kati) wa Manchester United na wenzake Victor Lindelof (kulia) na mshambuliaji Romelu Lukaku wafurahia mara baada ya kufuzu robo fainali Man U iliposhinda Paris Saint-Germain (PSG) Machi 6, 2019, uwanjani Parc des Princes. Picha/ AFP

“Ni aibu kubwa. Wanaajiri watu wanne ambao hawaelewi masuala ya soka kutazama video za mechi mbele ya runinga,” Neymar, ambaye alikuwa mkekani akiwa na jeraha na kutazama mechi katika eneo la mashabiki uwanjani Parc des Princes, alisema kwenye akaunti yake ya mtandao wa Instagram.

Kocha wa PSG, Thomas Tuchel alisema anahurumia Neymar kwa masikitiko yake.

“Wakati mwingine unatumia maneno ambayo unayameza saa chache baadaye,” alisema Tuchel.

“Unaona jinsi alitamani sana kutusaidia.”

Tuchel hakuamini macho yake vijana wake walivyoaga Klabu Bingwa mikononi mwa United. Alisema kubanduliwa kwao nje ni “unyama”, ingawa alikataa kulaumu wasimamizi wa mechi baada ya penalti iliyohitaji uamuzi wa VAR kuwapa Waingereza tiketi ya kusonga mbele.

“Mimi nashabikia VAR na sibadili msimamo wangu,” alisema Tuchel.

Baada ya kushinda 2-0 Februari, PSG iliyumba katika mechi ya marudiano, ingawa ilikuwa bado mbioni kutinga robo-fainali hadi pale refa kutoka Slovenia Damir Skomina alipoamua Presnel Kimpembe alinawa mpira ndani ya kisanduku baada ya VAR kutumika kurejelea tukio hilo.

Diogo Dalot

Shuti la Diogo Dalot lilimpiga mkono Kimpembe, na Rashford akafunga penalti hiyo kuweka United ndani ya nane-bora kupitia bao la ugenini.

“Kivyangu, niliona Dalot akipiga shuti. Niliona mpira ukipaa kutoka mguu wake na kwangu mimi, ulikuwa unaelekea nje,” alisema Tuchel.

“Kuna mambo mengi ya kujadili kabla ya kufanya uamuzi na ninadhani ulikuwa uamuzi wa asilimia 50-50.

“Kinachofanya uamuzi kutokuwa sawa ni kwamba nahisi shuti hilo lilikuwa linaenda nje na kuamua ni penalti, ni jambo lisilofaa.”

Mabao mawili kutoka kwa Romelu Lukaku katika kipindi cha kwanza yalifufua matumaini ya United, lakini Juan Bernat alirejesha goli moja na kuweka PSG pazuri.

Tuchel aliongeza, “Unaweza kusema tulicheza katika hatari hii kwa dakika 60 tukijua kwamba tusipofunga, tunaweza kujuta.”