Bajeti kuipiga jeki miradi yote mikuu ya Pwani

Bajeti kuipiga jeki miradi yote mikuu ya Pwani

Na ANTHONY KITIMO

ENEO la Pwani linatarajiwa kupiga hatua kubwa katika ujenzi wa baadhi ya miradi mikuu ya miundomsingi inayoendelezwa na serikali kuu.

Hii ni baada ya miradi iliyo chini ya ajenda nne kuu za Rais Uhuru Kenyatta katika eneo hilo, kutengewa zaidi ya asilimia 37 ya bajeti ya wizara ya uchukuzi mwaka wa kifedha wa 2021/2022.Hali hii inaashiria kuwa, serikali imo mbioni kupiga hatua katika ujenzi wa miundomsingi kabla hatamu ya Rais Kenyatta ikamilike miezi 14 ijayo.

Mradi utakaonufaika zaidi ni ujenzi wa eneo maalumu la kiuchumi la Dongo Kundu. Ni mara ya kwanza mradi huo kuwahi kutengewa fedha katika bajeti ya taifa.Mradi huo umetengewa Sh8.5 bilioni, na ni wa pili kupata mgao mkubwa zaidi baada ya mradi wa reli ya SGR kutoka Nairobi hadi Naivasha ambao ulitengewa Sh27 bilioni.

Kwa jumla, wizara ya uchukuzi imetengewa Sh53.5 bilioni.Hatua hii inatarajiwa kuwezesha ujenzi wa eneo maalumu la kiuchumi la Dongo Kundu kuanza kwani mradi huo ulikwama tangu uzinduzi wa ujenzi ulipofanywa mnamo Oktoba 18, 2019.

Mradi huo ambao unatekelezwa kwa awamu tatu unatarajiwa kuwezesha Mombasa kuwa kitovu cha sekta ya viwanda ambacho kitavutia biashara nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki na ya Kati.

Katika bajeti ya mwaka wa 2021/2022, Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) inatarajiwa kukamilisha miradi mingi baada ya kutengewa Sh7.5 bilioni.Kiwango hicho kimeongezeka kwa zaidi ya Sh2.5 bilioni ikilinganishwa na mwaka uliopita wa kifedha.

Miongoni mwa miradi ambayo imepewa kipaumbele katika bandari ya Mombasa ni kukamilishwa ujenzi wa kituo cha pili cha kupakua makasha, ambacho kitaongezea bandari uwezo wa kushughulikia kiwango kikubwa cha mizigo na mafuta kufikia Januari 2022.

Kulingana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Bw Rashid Salim, kituo hicho kipya kitakuwa na uwezo wa kupokea meli nne kwa wakati mmoja ikilinganishwa na kituo cha sasa ambacho hupokea meli moja pekee.

Hata hivyo, katika bajeti hiyo, mradi wa Uchukuzi kutoka Bandari ya Lamu-Sudan Kusini-Ethiopia (Lapsset) umepunguziwa bajeti kwa mwaka wa pili sasa.Bajeti ya Lapsset imepunguzwa kwa zaidi ya Sh2 bilioni ikilinganishwa na mwaka uliopita, na mradi huo sasa umetengewa Sh4.4 bilioni.

Mwezi uliopita, Rais Kenyatta aliongoza uzinduzi wa sehemu ya kwanza inayotumiwa na meli kupakia na kupakua mizigo bandarini Lamu.Bandari hiyo inapangiwa kuwa na gati 32 kwa jumla. Ujenzi wa gati ya pili na ya tatu unatarajiwa kukamilishwa Julai na Oktoba mwaka huu, kwa mujibu wa Rais.

Serikali imepunguza pia fedha zilizotengewa bima ya shirika la huduma za feri kwa takriban asilimia 50, kutoka Sh328 milioni hadi Sh128 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Sh14b zatengewa kukabili corona

Kilimo chatengewa Sh60b