Habari Mseto

BAJETI: Waiguru akatwa miguu na MCAs

July 1st, 2020 1 min read

Na GEORGE MUNENE

MADIWANI wa Kirinyaga sasa wameamua kutumia mamlaka yao kumwadhibu Gavana Anne Waiguru kwa kumpunguzia mgao wa fedha katika bajeti.

Madiwani hao Jumanne waliamua kupunguza fedha za kulipa mawakili wa kaunti hiyo kutoka Sh60 milioni hadi Sh1 milioni.

Walidai kuwa, fedha zilizotengwa kulipa mawakili hao wanapowakilisha kaunti katika kesi mbalimbali kortini zilikuwa nyingi mno.

Waliamua kuelekeza fedha hizo katika idara ya elimu na kukabidhi zingine kwa ofisi ya Naibu Gavana Peter Ndambiri ambaye awali hakuwa na mgao wowote wa fedha.

Wakati wa kupitisha bajeti ya Sh5.5 bilioni ya mwaka wa fedha wa 2020/2021, wawakilishi hao walisisitiza kuwa watahakikisha fedha za umma zinatumika vizuri.

“Ilibidi tuchukue hatua wakati tuligundua kuwa ofisi ya naibu gavana haijatengewa hela zozote na serikali ya kaunti. Ofisi hii ni muhimu na haiwezi kufanya kazi bila fedha,” akasema Bw David Mathenge, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge ya kaunti hiyo.

Uhasama wa kisiasa kati ya Bw Ndambiri na Gavana Waiguru umekuwa ukionekana wazi katika siku za hivi majuzi.

Kando na hayo, madiwani walisababisha pigo kubwa kwa ofisi ya Katibu wa Kaunti na hivyo kulemaza shughuli za gavana, baada ya kupunguza bajeti ya katibu huyo kutoka Sh111 milioni hadi Sh1 milioni pekee.

“Tumekuwa tukimwomba katibu wa kaunti atupe hati za kutusaidia kuweza kutekeleza jukumu letu la kuangalia kuwa serikali ya kaunti inafanya kazi ipasavyo, lakini amekuwa akidinda. Kwa hivyo, tumelazimika kuipa ofisi yake kiwango kidogo cha fedha,” akasema Bw Mathenge.

“Katibu wa Kaunti amekuwa akifanya kazi yetu kuwa ngumu sana na Gavana amekataa kumfuta kazi,” aliendelea.

Pia, Sh500,000 zilizotengewa Idara ya Mawasiliano ya gavana pia ziliondolewa na kuelekezwa kwa maendeleo ya kaunti.

Wawakilishi hao wa wadi walisema idara hiyo imekuwa ikitumika kama chombo cha kueneza propaganda na kwa hivyo haifai kupata asilimia yeyote ya fedha.