HabariSiasa

BAJETI YA KUNYONYA: Raia kuumia zaidi

June 14th, 2018 2 min read

CHARLES WASONGA na VALENTINE OBARA

BEI ya unga, maziwa, mkate, mafuta taa na bidhaa nyingine za kimsingi itapanda Bunge likipitisha Mswada wa Mabadiliko ya Sheria za Ushuru ambao utatumiwa kutekeleza bajeti iliyosomwa Alhamisi.

Kulingana na mswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya pili jana bungeni, serikali inapania kuongeza kiwango chake kwa ukusanyaji ushuru kwa kutoza watengenezaji wa bidhaa za kimsingi ushuru wa thamani ya ziada (VAT). Hii inamaanisha nao watapitisha gharama hiyo kwa watumiaji bidhaa hizo.

Bidhaa za kimsingi kama vile unga, hazijakuwa zikitozwa ushuru wa VAT chini ya sheria ya sasa kuhusu ushuru.

“Mswada huo unalenga kuiwezesha serikali kukusanya ushuru zaidi ili iweze kupata pesa za kufadhili mipango yake ya maendeleo. Dhima kuu ni kuhakikisha kuwa serikali inapata pesa za kutekeleza nguzo zake nne za maendeleo,” akasema Naibu Kiranja wa Wengi, Bi Cecily Mbarire alipowasilisha mswada huo kabla ya waziri Henry Rotich kuwasili bungeni.

Bw Rotich alirejela mswada huo kwenye taarifa yake alipoutetea akisema utarahisisha kiwango na kasi ya ukusanyaji ushuru.

“Mswada wa mabadiliko ya ukusanyaji ushuru utarahisisha mfumo wa ukusanyaji ushuru, hali ambayo itaimarisha mapato ya serikali. Vile vile, utarahisisha ukusanyaji wa ushuru wa VAT ili serikali ipate fedha za kufadhili utekelezaji wa nguzo nne kuu za maendeleo,” akasema Bw Rotich.

Kupitishwa kwa mswada huo kutamaanisha kuwa bei ya unga itapanda kutoka wastani wa Sh100 kwa sasa hadi takriban Sh120 kwa paketi moja ya kilo mbili.

Bei za mkate na maziwa pia zitakwenda juu kutoka wastani wa Sh50 hadi zaidi ya Sh60.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge, Bw John Mbadi, alisema mrengo wa upinzani utapinga vikali hatua ya serikali ya kuongeza bei ya bidhaa za kimsingi ambazo hutumiwa na Wakenya wote, wengi wao wenye mapato ya chini.

“Hii sio bajeti ya mwananchi kwa sababu inalenga kuongeza ushuru unaotozwa bidhaa za kimsingi kama vile unga, maziwa na mafuta taa. Tutapinga mipango yote ya serikali ya kumbebesha mwananchi wa kawaida mzigo wa gharama ya maisha kwa kumwongezea ushuru, aidha kupitia makadirio ya bajeti, mswada wa fedha au huu mswada wa mabadiliko ya sheria za ushuru,” akasema Bw Mbadi.

Waziri Rotich pia alipandisha ushuru unaotozwa mafuta taa na kuuweka kiwango sawa na ule unaotozwa petroli na gesi ya kupikia, akisema hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi ya mafuta taa.

“Tumesawazisha ushuru unaotozwa mafuta taa na ule wa petroli na gesi ya kupikia ili kupunguza matumizi yake ambayo husababisha uchafuzi wa hewa, “ akasema Bw Rotich.

Ushuru wa mafuta taa utaongezwa kutoka Sh7,205 hadi Sh10,305 kwa kila lita 1,000, gharama ambayo inatarajiwa kupitishwa kutoka kwa wafanyabiashara hadi kwa wateja wadogo.

Hii ina maana kuwa wananchi haswa wenye mapato ya chini ambao hutumia mafuta taa kupikia na kwenye mataa yao wataumia zaidi.

Kwa upande mwingine, ushuru unaotozwa kwa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa simu utaongezwa kutoka asilimia 10 hadi 12.

Mbali na hayo, bidhaa nyingi zinazoingizwa nchini kutoka nchi za kigeni kwa bei nafuu pia zitaongezwa ushuru.

Bw Rotich alipendekeza nguo na viatu vya mitumba pamoja na mavazi mengine yanayoingizwa nchini kutoka nchi za kigeni zitozwe ushuru wa asilimia 35.

Kulingana na waziri, hatua hii ambayo imechukuliwa pia kwa bidhaa zingine kutoka mataifa ya kigeni kama vile mafuta ya kupikia, mbao na fanicha, dawa za wadudu na karatasi na bidhaa zake kama vile vitabu, imenuiwa kulinda sekta ya viwanda nchini.

“Hatua hizi pia zinalenga kufanya bidhaa zetu zipate soko na wakati huo huo kulinda viwanda vyetu kutokana na ushindani usio wa haki kutoka nje,”

akasema.