Michezo

BALAA LEO: Liverpool yahitaji muujiza ugani Anfield kuzima Barcelona UEFA

May 7th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, UINGEREZA

BARCELONA wanatarajiwa kuwa kikosi cha kwanza kufuzu kwa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Miamba hao wa soka ya Uhispania watatua uwanjani Anfield kurudiana na Liverpool katika mchuano wa mkondo wa pili wa nusu-fainali.

Kubwa zaidi linalowafanya Barcelona kupigiwa upatu wa kutinga fainali kirahisi ni ushindi mnono wa 3-0 waliousajili dhidi ya Liverpool katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha ugani Camp Nou mapema wiki jana.

Ingawa hivyo, kocha Ernesto Valverde amewaonya masogora wake dhidi ya utepetevu ambao huenda ukawachochea Liverpool kuchuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani.

“Wengi wanatarajia Barcelona wawe na wakati mwepesi dhidi ya Liverpool ugenini. Hali huenda isiwe hivyo hasa ikizingatiwa hamasa ambayo wenyeji wetu wanatarajiwa kupata kutoka kwa mashabiki wao,” akasema Valverde.

Ili kuwapa masogora wake fursa nzuri ya kujiandaa kwa mechi dhidi ya Liverpool, Valverde ambaye tayari amewaongoza Barcelona kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), aliwapumzisha nyota wote kikosini mwake wikendi jana.

Hatua hiyo iliwafanya Barcelona kupokezwa kichapo cha 2-0 na wenyeji wao Celta Vigo.

Hivi leo Jumanne, Barcelona wanatazamiwa kuwarejesha kikosini wachezaji Marc-Andre ter Stegen, Gerard Pique, Clement Lenglet na Jordi Alba huku beki wa kulia Nelson Semedo akipigiwa upatu wa kuanzishwa katika kikosi cha kwanza badala ya Sergi Roberto.

Huenda pia Valverde akachochewa kumwajibisha kiungo Arturo Vidal kwa lengo la kushirikiana na Ivan Rakitic au Sergio Busquets katika safu ya kati.

Uwepo wa Vidal katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliwapa Barcelona fursa mwafaka ya kuvurugika uthabiti wa ngome ya Liverpool.

Uteuzi wa Valverde wa kumwajibisha Vidal kwa dakika 30 pekee dhidi ya Celta Vigo mwishoni mwa wiki jana ni dalili zilizoashiria uwezekano wa kiungo huyo mzawa wa Chile kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Barcelona itakapokipiga usiku dhidi ya Reds.

Chipukizi Ousmane Dembele hatakuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona baada ya fowadi huyo mzawa wa Ufaransa kupata jeraha lililomshuhudia akiondolewa mapema uwanjani dhidi ya Celta Vigo.

Dembele

Kutokuwepo kwa Dembele kutamsaza Valverde katika ulazima wa kumwajibisha Philippe Coutinho kwa mara nyingine dhidi ya waajiri wake wa zamani.

Kwa pamoja na Luis Suarez aliyekuwa mfungaji wa bao la kwanza la Barcelona dhidi ya Liverpool wiki jana, Coutinho pia anatazamiwa kukaribishwa kwa matusi ya kila aina ugani Anfield hasa ikizingatiwa kwamba aliagana na miamba hao wa soka ya Uingereza wakati ambapo walikuwa bado wanamhitaji zaidi.

Suarez na Messi ambaye alifunga mabao mawili dhidi ya Liverpool katika mchuano wa mkondo wa kwanza, wanatarajiwa kuongoza safu ya mbele ya Barcelona ambao wanafukuzia jumla ya mataji matatu msimu huu.

Wapambe hao wa soka ya Uhispania wamepangiwa kuchuana na Valencia katika fainali ya kuwania ubingwa wa taji la Copa del Rey mnamo Mei 25.

Kwa upande wao, Liverpool watakosa huduma za fowadi Roberto Firmino. Kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp huenda pia kikakosa huduma za mvamizi Mohamed Salah aliyepata jeraha baya la kichwa dhidi ya Newcastle United katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa wiki jana.