Balaa mikopo ya Kenya ikifika Sh9tr

Balaa mikopo ya Kenya ikifika Sh9tr

Na DAVID MWERE

RAIS Uhuru Kenyatta sasa atahitaji idhini ya Wabunge kabla ya kukopa fedha kutoka kwa taasisi za humu nchini na mataifa ya kigeni baada ya kufikisha kiwango cha juu cha deni.

Oktoba 2019, Bunge liliruhusu serikali kukopa hadi pale deni la kitaifa litakapofikia Sh9 trilioni.

Serikali imesalia na chini ya Sh1 bilioni kabla ya deni la kitaifa kufika Sh9 trilioni. Hiyo inamaanisha kuwa serikali ikitaka kukopa ni sharti ipate idhini kutoka kwa bunge.

Katika hali hiyo, italihitaji Bunge kuidhinisha mpango wowote wa serikali kukopa fedha zinazozidi Sh1 bilioni.

Waziri wa Fedha, Ukur Yatani, tayari amekubali kuwa serikali itahitajika kukopa zaidi ili kufadhili bajeti yake ya Sh3.66 trilioni ya mwaka wa kifedha wa 2021/22.

Ili kufikia hilo, itahitaji Mswada wa Matumizi ya Fedha za Umma kufanyiwa mageuzi ili kuongeza kiwango inachoweza kukopa kutoka Sh9 trilioni hadi Sh12 trilioni.

Ripoti ya Kamati ya Uhasibu Bungeni (PAC) na ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Makadirio ya Bajeti (BAC) mwaka uliopita, ziliizuia Wizara ya Fedha dhidi ya kuwasilisha nyongeza ya bajeti mara kwa mara katika Bunge.

Kukubaliwa kwa ripoti hizo mbili kunamaanisha Wizara itazuiwa kuwasilisha nyongeza hizo miezi miwili kabla ya mwaka wa kifedha kuisha. Mwaka wa kifedha wa serikali huwa unaanza Julai 1 hadi Juni 30 kila mwaka.

Athari za mapendekezo ya ripoti hizo mbili ni kwamba hakuna nyongeza ya bajeti itakayowasilishwa bungeni baada ya Aprili 30.

Kipengele 223 cha Katiba kinafafanua kuhusu hali ambapo nyongeza ya bajeti inapaswa kuwasilishwa katika Bunge. Katika hali hiyo, BAC imeonya kuwa huenda bajeti ya mwaka huu isitimize malengo yake.

Hata hivyo, mapendekezo ya kamati hizo mbili yataanza kutekelezwa ikiwa Bunge litaufanyia mageuzi Mswada wa Matumizi ya Fedha za Umma (PFM).

Mbunge Opiyo Wandayi (Unguja), ambaye ndiye mwenyekiti wa PAC, alisema kamati hiyo tayari ishaandaa marekebisho ya mswada huo inaolenga kuwasilisha bungeni wiki ijayo.

“Kupitishwa kwa mswada huu kutahakikisha nchi haitaendelea kuchukua mikopo ambayo huenda ikawa vigumu kuilipa baadaye kutokana na kiwango cha chini cha ukusanyaji wa ushuru,” akasema Bw Wandayi.

Ripoti inasema lazima idhini ya kuchukua mikopo kama hiyo itolewe na Bunge kabla ya serikali kubuni mikataba na mashirika ya kifedha.

Hali hiyo inajiri wakati Halmashauri ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA) inakumbwa na changamoto kufikisha malengo yake.

Ripoti maalum iliyotayarishwa na Wizara ya Fedha inaonyesha kuwa kufikia Desemba 2020, deni la nje la Kenya lilikuwa limefikia Sh7.3 trilioni.

Hata hivyo, ripoti nyingine iliyotolewa majuzi na Afisi ya Bunge kuhusu Bajeti ilionyesha kuwa deni la taifa lilikuwa limefikia Sh8.4 trilioni.

Afisi hiyo imekuwa ikieleza wasiwasi wake kuhusu mtindo wa serikali kuchukua mikopo ya nje bila idhini ya Bunge.

Taarifa maalum kuhusu bajeti iliyowasilishwa Bungeni inaonyesha kuwa serikali inapanga kukopa angaa Sh1 trilioni kutoka taasisi za kifedha nchini ili kujaza pengo lililopo kwenye bajeti.

You can share this post!

Kocha Allegri awataka Juventus wamsajili upya kiungo Paul...

Ujanja wa magavana wenye kesi kuendelea kuhudumu