Michezo

BALAA: Tottenham Hotspur yarambishwa sakafu na Colchester United

September 26th, 2019 2 min read

LONDON, Uingereza

COLCHESTER United ilifanya maangamizi makubwa ya kushangaza kwa kuibandua mapema Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutoka michuano ya Carabao Cup, Jumanne usiku.

Klabu hiyo ya Daraja la Pili iliibuka na ushindi wa 4-3 kupitia kwa mikwaju ya penalti katika mechi hiyo na kufuzu kwa raundi ya 16 bora. Penalti zilipigwa kuamua mshindi baada ya mechi hiyo kumalizika kwa 0-0 katika muda wa kawaida.

Ulikuwa usiku wa majonzi kwa Spurs ambao walitinga hatua ya nusu-fainali msimu uliopita. Ndoto za Spurs ziliangamia baada ya Cristian Eriksen na Lucas Moura kushindwa kufunga mikwaju yao.

Eriksen alikuwa wa kwanza kupiga penalti ambayo ilinyakwa na kipa Dean Gerken huku ya Moura ikipiga mlingoti wa goli na kutoka nje. Ilikuwa mara yao ya kwanza kutinga hatua hiyo ya 16 bora katika kipindi cha miaka 44.

Tangu ajiunge na Spurs, kocha Mauricio Pochettino hajafanikiwa kutwaa taji lolote, licha ya kuwa na kikosi imara msimu uliopita wa 2018-19 ambacho kitinga fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kabla ya kushindwa na Liverpool.

Chini ya ukufunzi wake, Spurs haijawahi kushindwa na timu ndogo katika mechi 18 tangu awasili 2013 akitokea Southampton.

Dhidi ya Colchester, Pochettino alifanya mabadiliko 10 kwenye kikosi chake kilichoshindwa majuzi na Leicester. Ni kipa Gazzaniga pekee aliyehifadhi nafasi yake kikosini.

Eric Dier alicheza mechi hiyo akijaza nafasi ya Dele Ali baada ya kupata nafuu kutokana na jeraha, na pia ilikuwa mechi ya kwanza kwa makinda Japhet Tanganga na Troy Parrott wenye umri wa miaka 20 na 17, lakini hawakufana.

Spurs wamecheza mechi tano ugenini bila ushindi. Ushindi mara nne pekee katika mechi 17 ni jambo linalowapa mashabiki wa klabu hiyo wasiwasi tele.

 

Wachezaji wa Tottenham Hotspur katika mchuano wa awali. Spurs walilambishwa sakafu na klabu limbukeni ya Colchester United katika Kombe la Carabao siku ya Jumanne, Septemba 24, 2019. Picha/ AFP

Ulikuwa ushindi wa pili wa kushangaza kwa Colchester ambayo awali iliibuka na ushindi mwingine dhidi ya Crystal Palace katika hatua ya raundi ya pili.

Colchester imekuwa klabu ya kwanza kutoka daraja la chini kushinda timu mbili za EPL katika michuano ya Carabao Cup tangu Bradford City ifanye hivyo msimu wa 2012-13.

Timu kubwa mara nyingi hutumia michuano hii kuwapa nafasi wachezaji chipukizi, lakini jinsi walivyocheza, huenda vijana wa Colchester chini ya kocha John McGreal wakaendelea kuangusha vigogo.

Aliyekuwa kocha wa Bolton, Owen Coyle ni miongoni mwa watu mashuhuri wanaoamini kwamba Spurs ambayo iko nyuma ligini kwa mwanya wa pointi 10 dhidi ya vinara Liverpool itazidi kudidimia.

Spurs watarejea uwanjani mwishoni mwa wiki kucheza na Southampton katika pambano la EPL Jumamosi, wakati Colchester wakiwa ugenini dhidi ya Macclesfield, pia siku hiyo katika mechi yao ya Ligi Daraja la Pili.