Michezo

Balaji EPZ, KNH na Mwiki United zatisha ligi daraja la pili

March 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

BALAJI EPZ, timu ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta(KNH) na Mwiki United zinazidi kuwasha moto kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu.

Kikosi cha KNH kiliichoma Commercial FC magoli 3-0 wakati Mwiki United ikifunga Thika Allstars mabao 2-0. Nayo Balaji EPZ iliendelea kutamba ilipozoa alama zote ilipocharaza Kahawa United bao 1-0.

Kwenye jedwali timu hizo zinafunga tatu bora zikifuatana kwa usajari huo.

KNH ya George Makambi ilivuna ugenini baada ya kudhalilisha Magana Flowers kwa magoli 6-2 wiki iliyopita.

Chini ya nahodha Ben Obiri KNH iliwazidi maarifa wenyeji wao na kufanya kweli kupitia Alassane Lass, Peter Njama na Sibomona Siboh waliopiga moja safi kila mmoja. ”Kama nilivyosema wiki iliyopita tumepangwa Kundi la kifo kuteleza tu utaachwa kwa mataa,” kocha huyo alisema huku akipongeza vijana wake kwa kazi nzuri.

Nao John Kimani na Francis Nyoike kila mmoja alitikisa nyavu mara moja na kubeba kunyamazisha Thika Allstars huku Uweza FC ikilazimisha sare ya mabao 2-2 na Kenafric FC. Mechi zingine, Jumbo T ilibanwa mabao 2-1 na Zetech University nayo Limuru Olympics ilinasa mabao 2-0 mbele ya Magana Flowers.