Michezo

Balaji EPZ na Equity Bank FC na Gor Mahia Youth zitatamba tena msimu huu?

July 16th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

KAMPENI za kufukuzia ubingwa wa Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu unaokamilika zilishuhudia mitifuano mikali kinyume na matarajio ya wengi na kutoa picha kamili kuwa michezo hiyo inaimarika kila mwaka. Jumla ya timu 38 zilishiriki mechi za kupigania ubingwa wa kipute hicho msimu wa 2018/2019 zilizogawanywa mara tatu Kundi A, B na C.

Katika mpango mzima wachezaji wa Balaji EPZ na Equity Bank FC wamejaa tabasamu tele baada ya kunasa ubingwa wa mechi za Kundi A na Kundi B bila kuweka katika kaburi la sahau bingwa wa Kundi C Gor Mahia Youth.

Hata hivyo huku mabingwa hao wakishangilia kwa furaha wengine nao wanaendelea kununa baada ya kulemewa kunasa tiketi za kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki soka la hadhi ya juu msimu ujao.

Mabingwa hao wameketi katika mkao wa subira kupandishwa ngazi kushiriki mikwaruzano ya ubingwa wa Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu ujao.

Hata vikosi vingine vinasubiri neema ya Mungu ivishukie kubahatika kupata nafasi ya kusonga mbele kushiriki michuano hiyo. Mfano Butterfly FC iliyomaliza ya pili Kundi C na timu ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) iliyokuwa Kundi A kila moja imetegea muujiza wake Mungu. KNH ilionyesha mchezo safi na kuimarika kwa asimilia fulani ambapo ilimaliza ya pili kinyume na misimu iliyopita.

Siku chache kabla ya mechi hizo kufikia tamati kocha wa KNH alisema ”Mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Pili zimetuchosha baada ya kushiriki miaka kadhaa tunatamani zaidi kunasa tiketi ya kufuzu kushiriki soka la hadhi ya juu msimu ujao.”

Nakumbuka mwanzoni mwa mechi hizo, kocha wa KNH alinukuliwa akisema kuwa michuano hiyo iliyoshuhudia ushindani mkali kinyume na matarajio ya wengi. Namnuu ”Kusema kweli tumepangwa kundi la kifo timu moja ikiteleza tu nyingine inapenya kama risasi kamwe hakuna kulala dimbani,” alisema.

Balaji EPZ iliibuka mabingwa wa Kundi A baada ya kukusanya alama 46, moja mbele ya KHN. Nafasi ya tatu iliendelea timu ya Zetech University ya kocha, Bernard Kitolo kwa kuvuna pointi 40, moja mbele ya Uweza FC kati ya vikosi vilivyopigiwa upatu kutesa kwenye michezo hiyo.

Taji la Kundi B liliendea Equity Bank FC kwa kutwaa pointi 50, 11 mbele ya Kariobangi Sharks B FC, huku baada ya kuzoa alama 36, Shofco Kibera ilimaliza tatu bora. Kundi C taji lilibebwa na Gor Mahia Youth kwa alama 57 nayo Butterfly FC iliibuka ya pili kwa kufikisha alama 48, tatu mbele ya Tandaza FC.

”Wadau wa soka nchini napaswa kufahamu mambo kadhaa kwenye michuano ya Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu wa 2018/2019 maana washiriki wapya katika makundi yote tatu ndiyo waliofaulu kutwaa ubingwa huo,” meneja wa Butterfly FC, Fredrick Ndinya alisema na kuongeza hatua hiyo inaonyesha wazi kwamba mchezo wa Kenya kiasi unaopiga hatua.

Hata hivyo anaponda waamuzi wa mechi za ligi wenye kasumba potovu ambapo hupenda kuzibeba timu zinazohusiana na baadhi ya viongozi wa michezo tofauti nchini kulalia wapizani wao kwa kutoa maamuzi yasiofaa.