Habari

Balala alaumu Bandari, CFS kwa ulanguzi wa mihadarati

October 24th, 2019 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala amelaumu Bandari ya Mombasa na sehemu za kuhifadhi makasha (CFS) akidai zinatumika kupitishia bidhaa haramu zikiwemo dawa za kulevya.

Akihutubia wawekezaji kutoka mataifa 24 ya Afrika na Ulaya kuhusu vita dhidi ya ulanguzi wa pembe za ndovu Jumatano jijini Mombasa, Bw Balala pia alisema maeneo hayo hutumika kupitishia bidhaa haramu za wanyamapori.

“Serikali sasa itahakikisha kuwa makasha yanayofikishwa bandarini yanakaguliwa kwa kina kabla ya kusafirishwa maeneo ya bara,” akasema Bw Balala.

Alisema biashara haramu ya uwindaji wanyama wa porini, ulanguzi wa dawa za kulevya na ukwepaji wa ushuru ni miongoni mwa uhalifu unaoshuhudiwa katika soko la humu nchini.

Alieleza kuwa ulanguzi wa dawa za kulevya unaendelea kuharibu vijana wengi Pwani na sharti uovu huo ukomeshwe.

“Hatutaki kuzungumzia suala la Bandari ya Mombasa ambayo inatumika kama sehemu ya biashara za magendo. Lakini dawa za kulevya zinamaliza jamii, mazingira na hata tamaduni zetu. Hatuwezi kukubali biashara hizo ziendelezwe,” alisema.

Aliwahakikishia wawekezaji hao kwamba Rais Uhuru Kenyatta yuko mbioni kuangamiza biashara zote haramu.

Lakini afisa mkuu wa Muungano wa wenye CFS, Bw Daniel Nzeki alipinga madai ya Bw Balala.

“Hakuna mmiliki wa CFS anayejihusisha na biashara haramu kwa sababu sehemu hizo hukaguliwa na serikali,” akasema Bw Nzeki.

Lakini Bw Balala alisitiza kuwa biashara hiyo inaendelezwa kimagendo akisisitiza ufisadi umechangia pakubwa.

“Licha ya serikali kuwekeza katika sekta ya usalama wa bandarini na teknolojia za kunasa bidhaa ghushi, ufisadi unahujumu juhudi hizi,” alisema waziri.

Pia aliwashtumu waandamanaji wanaoendeleza maandamano Mombasa kila jumatatu wakilalamikia kuzoroteshwa kwa uchumi wa Mombasa.

Wafanyibiashara na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu wamekuwa wakiandamana wakisema uchumi wa Mombasa umezoroteshwa na sheria za serikali.

“Hawaelewi kinachoendelea ama wanataka tu kuzua vurugu,” alisema na kuwataka wamiliki wa CFS na wenye malori wabadilishe mbinu za kibiashara.