Habari

Balala lawamani kuhusu makavazi

March 12th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Utalii Bw Najib Balala yuko lawamani kwa kuendelea kushinikiza kubuniwa kwa Makavazi ya Jamii ya Waswahili tangu mwaka 2017, bila kutekeleza hatua hiyo.

Licha ya kuwa serikalini, Bw Balala amekuwa akishinikiza hilo, hali inayoibua maswali kuhusu sababu ambapo hajachukua hajafanikisha utekelezaji wa hatua hiyo.

Mnamo Jumatatu, waziri alieleza haja ya kubuniwa kwa makavazi hayo, akisema kuwa yatachangia sana kukuza utamaduni wa jamii hiyo.

“Ninaunga mkono kubuniwa kwa Makavazi ya Jamii ya Waswahili. Kumbuka kwamba makazi ya Waswahili yalianza kujengwa katika karne ya tisa, kulingana na historia. Tunahitaji kuhifadhi historia yetu na utamaduni wa Waswahili,” akasema.

Hiyo ilikuwa mara ya tatu kwake kutoa kauli hiyo, ikizingatiwa alifanya hivyo kwenye hafla aliyohudhuria na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni na Michezo Bw Hassan Wario.

Vilevile, alisema kuwa hatua hiyo ingechangia sana kuwavutia watalii katika eneo la Pwani.

Kwenye hafla hiyo ya 2017, ambapo aliongoza ufunguzi wa Jumba Maalum la Oman na Ukumbi wa Maonyesho wa Mazrui, Bw Balala aliahidi kwamba angetoa Sh5 milioni kusaidia kwenye ujenzi wa makavazi hayo.

Mfanyabiashara Suleiman Shahbal pia aliahidi kutoa kiasi kama hicho cha kufadhili ujenzi huo.

Kauli yake inaonekana kuendeleza tabia ya wanasiasa kutoa ahadi hewa, huku wakikosa kuzitekeleza licha ya kuwa serikalini.

Hili pia ni licha ya wizara zao kutengewa mamilioni ya pesa kufadhili miradi muhimu.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji katika Sekta ya Utalii (KTF) Bw Mohamed Hersi, alisema kuwa, licha ya ucheleweshaji huo, ni hatua nzuri kwani serikali imeonyesha umuhimu wa makavazi hayo.

“Tunapaswa kuipa serikali muda. Sijalifuatilia suala hilo kwa kina ingawa ninaami kuwa kuna mipango ya kulitekeleza ikiwa waziri mwenyewe amelitaja,” akasema Bw Hersi, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’.

Pwani ni mojawapo ya maeneo ambayo yana vivutio vingi vya watalii, baadhi yakijumuisha majengo ya kihistoria.

Miongoni mwa vivutio hivyo ni Ngome ya Fort Jesus, majengo ya kikale katika kisiwa cha Lamu, vyakula vya Waswahili kati ya mengine.

Sekta hiyo pia ni mojawapo ya zile zinazochangia sana katika ukuaji wa pato la jumla la taifa.

Kulingana Halmashauri ya Kitaifa ya Kukusanya Takwimu (KNBS) sekta hiyo inarajiwa kuchangia Sh964 bilioni kwa pato la taifa kufikia mwaka uliopita.

Kando na hayo, inatajwa kubuni nafasi za ajira 1.1 milioni mwaka 2019.